October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maro: Jiwe lishe kuongeza lishe kwa mifugo

JIWE lishe ni teknolojia iliyoibuliwa na kituo cha TALIRI Kongwa kilichopo kanda ya kati Mkoani Dodoma kwa lengo la kuwezesha mifugo kupata nguvu, protini na madini kutoka kwenye jiwe ambalo mnyama anaweza kulitumia kwa kulamba au kutafuna jiwe hilo

Hayo yameelezwa na Ezekiel Maro Afisa Mifugo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam ndani ya banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi yakiwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi Pa Biashara Na Uwekezaji”

Maro ameeleza kuwa jiwe hilo limetengenezwa kwa viini lishe mbalimbali yakiwemo mashudu ya alizeti, pumba za mahindi, chumvi na madini mbalimbali likiwa na uzito wa kilo tatu na linapatikana kwenye Kituo cha TALIRI Kongwa kwa gharama nafuu ambayo inamuwezesha mfugaji kumudu kulinunua.

“Jiwe hili linapaswa kuning’inizwa kwenye banda wanyama kama mbuzi, ng’ombe, kondoo yaani wanyama wote wanaocheua ili waweze kulifikia kwa kulamba au kutafuna” aliongeza Maro.

Aidha, Maro ameeleza kuwa tofauti ya jiwe hili na mawe mengine ni kuwa mawe mengine yana madini pekee ambayo yanakosekana kwenye chakula cha mifugo lakini jiwe hili vina viini lishe vyote muhimu ambavyo vitamuwezesha mnyama kupata lishe ambayo itamsaidia kuongeza uzalishaji kulingana na hali yake ya uzalishaji.

Tembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ujifunze teknolojia za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo.