November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Marekani kusaidia tafiti za magonjwa mbalimbali

Na Judith Ferdinand, Mwanza

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt.Donald Wright amesema,nchi yake ipo tayari kusaidia watafiti nchini hapa kufanya tafiti za magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani.

Dkt.Wright amesema hayo wakati alipotembelea na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na kuzungumza na waandishi wa habari,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mwanza.

Amesema, sehemu ya magonjwa tafiti ni muhimu sana,hivyo serikali ya Marekani itaendelea kuwaunga mkono watanzania wengi ambao wanataka kufanya tafiti katika magonjwa mbalimbali.

Pia amesema,Marekani inataka kutoa fedha katika nchi za Afrika kwa ajili ya kufanya tafiti ili kuwaunga mkono hususani zile zinazotaka kufanya tafiti sana sana kwenye nchi zao wenyewe.

Ambapo kwa upande wa Marekani vifo vinavyotokana na saratani vimepungua sana asilimia 30 mpaka 50, kwa sababu ya tafiti walizofanya na ela walizowekeza katika kufanya utafiti unao husiana na magonjwa ya saratani.

Sanjari na hayo,Marekani kuna Kitengo kinachoitwa National Institute for Health ambacho ndicho kinatoa fedha za kufanya tafiti zinazohusiana na magonjwa kama hayo.

“Kabla sijaja Tanzania kitengo hicho kiliniomba kukutana nacho ili tuweze kuzungumza ni jinsi gani wanaweza kutoa misaada kwa nchi ambayo ninakuja,nilifurahi kujua kwamba taasisi hiyo inafadhiri asilimia 78 kwa Tanzania pekee yake,tafiti hizi zipo katika nyanja mbalimbali lakini tumeweka msisitizo kwenye magonjwa ya UKIMWI na Malaria,”amesema Dkt.Wright.

Aidha amesema,moja ya kazi inayofanyika hospitali ya Muhimbili ambapo Balozi wa Marekani wanaifadhiri ni utafiti kuhusu sikoseli hivyo kwa ujumla serikali yao inatoa msaada katika maeneo hayo pamoja na kwenye saratani.

Pamoja na hayo amesema,Marekani ni watu wanaotoa kipaumbele sana katika masuala ya demokrasia ambapo miaka ya hivi karibuni wamekuja kugundua kwamba demokrasia nchini Tanzania imeonekana kushuka hasa ukiangali katika eneo la vyombo vya habari.

Amesema,kuhusu uhuru wa vyombo vya habari,kwa sasa vimemeanza kupata matumaini mapya tofauti na huko nyuma kwani upepo umeanza kurudi.

“Vyombo vya habari vimeanza kuwa huru pamoja na taasisi zingine za haki za binadamu hapa nchini tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita,vitu vyote havitaweza kubadilika kwa siku moja, lakini naona kuna matumaini makubwa ya kuwapo mabadiliko katika vyombo vya habari,”amesema.

Mbali na hayo amesema tayari ameishakutana na Waziri wa Habari , Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, Dkt.Ashatu Kijaji na kufanya naye mazungumzo na kwamba alionesha kutaka kufanya mabadiliko katika sekta ya habari nchini.

Pia amesema,Waziri huyo ametoa fursa kwa vyombo vya habari kuanisha vikwazo mbambali vinavyowakwamisha na kuviwasilisha kwake hadi kufikia Novemba 15, mwaka huu,ambapo majadiliano ni kitu muhimu katika kufikia muafaka na kwamba Dk. Kijaji ameonesha dhamira njema katika hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, amesema kutokana na mashirikiano mazuri ya Tanzania na Marekani,wamekuja kuangalia baadhi ya matunda ya matokeo ya mashirikiano hayo mazuri.

Mhandisi Gabriel,amesema pia Balozi huyo alitembelea taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu(NIMR) ambapo Marekani imeisha weka ufadhiri wake ambapo imeenda kukagua mradi wa malaria ambayo imekuwa ni ugonjwa ambao unaua mama na mtoto katika historia ya magonjwa hatarishi duniani lakini kwa kupitia tafiti, serikali ya Marekani imeweka mkono tafiti 78 zinazofanyika nchini ikiwemo ugonjwa wa malaria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko, amesema lengo kubwa la Balozi huyo wa Marekani ni kutambua mchango wa klabu hiyo iliyofanya kutetea haki ya wat kujieleza na uhuruwa vyombo vya habari.

Hii ni kutokana na MPC kuwa mstari wa mbele kufanya kazi na taasisi zilizo chini ya Ubalozi wa Marekani.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright,wa kwanza kushoto akimsikiliza Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko aliyesimama,wakati alipotembelea na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na kuzungumza na waandishi wa habari,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright,wa katikati waliokaa,akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko,wa kwanza kulia na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,kushoto pamoja na baadhi ya wanachama wa MPC wakati alipotembelea na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na kuzungumza na waandishi wa habari,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand