Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Mapango ya Amboni yanayosimamiwa na mamlaka ya hifadhi ya Mgorongoro yametajwa kuwa ndio pango pekee duniani ambalo dini zote hukutana sehemu moja na kufanya ibada jambo ambalo limeyafanya mapango hayo kuwa ya kipekee duniani kote.
Mapango hayo yametajwa kuwa ndio mapango pekee yanayotumika kwajili ya matambiko kwa mtu anayesumbuliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Asilimia kubwa ya watu wanatoka nje ya Mkoa wa Tanga kwajili ya kuja kufanya matambiko hayo .
Akizungumza mapangoni hapo Mhifadhi wa kituo cha mapango ya Amboni Mkoani Tanga Mecksadeck Mwambungu amesema kuwa wamekuwa wakipokea wageni wengi wakiwa na mbuzi na kuku kuanzia saa 12 asubuhi ambao wengi wao huwa wana ugomvi wa familia zao huku wengine wakija kuanzia saa 9 jioni kutoka maeneo ya Mikoani.
“Kitu kikubwa na ambacho ni cha maajabu ni kwamba hili ndio pango pekee duniani ambalo dini zote zinakutana sehemu moja na kufanya ibada bila kugombana wakiwemo wa dini ya kiislamu, wakristo na hata wasiokuwa na dini lakini hawagombani kila mmoja anafanya kwa nafasi yake na hakuna ugomvi wowote, “alisema
Aliongeza kuwa haya ni moja ya maajabu katika mapango yetu kwamba utakuta mganga wa kienyeji anachinja kuku pale na watalii wanapita kuendelea na shughuli zake hakuna mtu anayemuuliza mwenzake.
Mwambungu alisema katika pango la mzimu wa mabavu kuwa chimbuko la Afrika nzima kuhusiana na mila na desturi linapatikana mapangoni hapo kwa kuwa watu wanaoumwa na wenye matatizo yao wanakwenda kwenye pango hilo kwajili ya kuelezea shida zao ambapo wengi wao wamekuwa wakifanikiwa.
“Kama unavyoona kwenye pango hili kuna ramani ya Afrika hivyo chimbuko la mila na desturi linapatikana hapa kwa mfano una shida zako au umeumwa hujui umeumwa umwa vipi unakuja hapa lakini pia kuna waheshimiwa wengi wanakuja hapa hatuwezi kuwataja hata wabunge wanakuja unaweza kukuta amekuja leo na baada ya miezi 6 anarudi tena hii inaashiria kwamba wanafanikiwa, “alisema Mwambungu.
Alisema nchi nzima kwa yeyote anataka kufahamu Geography kwa vitendo anafika mapangoni hapo kwa kuwa kunapatikana vitu vingi vya kihistoria.
Akizungumzia historia ya pango namba 2 lililopewa jina la Fatuma linalotumika kwajili ya matambiko na wenyeji moungoza watalii Hamis Siwa amesema kuwa historia
“Katika mapango yetu 7 tunayoyahifadhi hili ni pango namba 2 na sababu ya pango hili kuitwa jina la Fatuma ni kwamba kuna mama mmoja hakufanikiwa kupata ujauzito kwa kipindi kirefu ambapo siku moja alilala na kuoteshwa kwamba aje sehemu hii aombe na baada ya kufika hapa akaomba akafanikiwa kupata ujauzito, “alisema.
Aliendelea kusimulia kuwa baada ya mama huyo kupata mtoto alioteshwa tena kuwa afike tena eneo hilo na mtoto na kumuita mtoto huyo Fatuma na hivi sasa huyo Fatuma ni mama mzee ambaye amekuwa akija hapa anakuja na familia yake wakiwa costa nzima na mbuzi kwajili ya kufanya matambiko japo kwa sasa tuna miaka kama mitatu sasa hatujamuona.
“Kuhusina na pango hili la Fatuma ni pango pekee linalotumika kwajili ya matambiko tuu kama una matatizo yako yanakusumbua na shida mbalimbali unakuja kwajili ya kufanyika matambiko na sio kwamba unakuja kufanya matambiko halafu ushindwe kufanikiwa hapana hivi vitu vinategemea unaweza ukaomba hapa usifanikiwe lakini ukaenda pango namba 1 la mzimu wa mabavu ukafanikiwa usipofanikiwa hapa kwa Fatuma damu yako inakuwa haijaendana na fatuma kwahiyo unakwenda pale mzimu wa mabavu, “alisema Siwa.
Siwa alisema kuwa watu wa pwani wana mwamko mkubwa ambapo wamekuwa wengi katika eneo hilo ambapo kwa siku wanapokea watu zaidi ya 10 ambao wanakwenda kufanya mambo ya matambiko.
Joyce Mgaya ni Meneja uhusiano mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro amesema kuwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kuboresha miundombinu katika mapango hayo licha ya hapo awali kuwepo kwa shughuli za kibinadamu kandokando ya mapango hayo.
“Nizidi kuwaomba waandishi wa habari muweze kuhamasisha na kuelimisha na kuhabarisha jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa uhifadhi katika maeneo ambayo serikali imeona kuna umuhimu wa kuhifadhi kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira bora na rafiki kwa vizazi vya sasa na vijavyo mmejionea wenyewe historia ambayo ipo hapa mkuu wa kituo amesema tunaweza kukaa zaidi ya mwezi tukisimulia kwamba kila pango lima historia yake, “alisisitiza Joyce.
Aidha aliwataka watanzania kujijengea utaratibu wa kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo nchini ikiwemo mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ili kuweza kujionea utalii unaopatikana Nchini.
Alisema watashirikiana na wadau mbalimbali wa utalii Mkoani Tanga ili kuweza kuibua vivutio ambavyp havifahamiki kwa kuvitangaza na kuviboresha miundombinu yake ili kuruhusu shughuli za kiutalii kuweza kufanyika.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu