January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maonesho ya Sabasaba mwaka huu funga kazi

*Kutumika kuionesha Dunia dhamira ya Rais Samia, ajira za muda
11,712 kupatikana, idadi ya washiriki ndani, nje usipime

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Dar

ZAIDI ya ajira za muda 11,712 zinatarajiwa kutengenezwa katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba ambapo yanatarajiwa kutembelewa na 353, 201.

Aidha jumla ya washiriki 3,846 wanatarajia kushiriki Maonesho hayo , ambapo washiriki wa ndani ni 3,433, kampuni za ndani sekta binafsi ni 3,286, Wizara nane, mikoa minne, halmashauri 30 na Taasisi za umma 102, nchi za nje 26 na kampuni za nje 413.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ,Exaud Kigahe, wakati akizungumza na waandishi wa habari,.
Amesema kwa mwaka huu ajira za muda zinazotarajiwa kutengenezwa takribani 11,687 na kufanya ongezeko la ajira takribani za muda 25 ukilinganisha na mwaka jana.

Amesema maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Julai 3, katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa , ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi akiwa na Mlezi wa maonesho hayo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Kigahe amesema kauli mbiu ya maonesho hayo ni Tanzania Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji ikilenga kuonesha Dunia kuwa Serikali ya awamu ya sita ipo tayari na inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara na kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji ikiwemo sekta ya viwanda, kilimo, teknolojia, uwekezaji na utalii.

Amesema maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake ambayo yamejikita katika teknolojia ya hali ya juu, ubunifu na matumizi ya akili mnemba (AI).

Amezitaja nchi za nje zilizothibitisha kushiriki ni pamoja na Korea, Uturuki, India, Japan, Singapore ,Syria ,Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Msumbijib,Indonesia, Mauritius, Oman, Misri, Iran , Pakistani, Rwanda ,Comoro, Zambia, Ethiopia na Kongo.

Ametaja nchi nyingine ni Ghana, China, Urusi, Italia, Uganda, Kenya na Zimbabwe.

Amesema nchi nyingi zinakuja kuonesha teknolojia mpya za mashine mbalimbali ambazo ni zile zinazohitajika na Watanzania katika kuanzisha viwanda vikubwa,vya kati na vidogo.

“Niwaombe wafanyabiashara wa ndani ya nchi kutumia fursa hiyo kujifunza kwaajili ya kuongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa pamoja na kupanga wigo wa masoko ya bidhaa zao,” alisema.

Amesema katika maonesho hayo kutakuwa na siku maalum ya nchi saba zinazoshiriki kwenye maonesho hayo ambazo ni China, Japan, Korea ,Iran, Misri, Urusi na India.

Kigahe amesema pia kutakuwa na programu ya Sabasaba Urithi wetu,programu za mikutano ya ana kwa ana,siku za kampuni zinazojumuisha sekta mbalimbali ambazo zimeandaliwa kwa kushirikiana baina ya sekta binafsi na sekta ya umma.

” Lengo la siku hizo za kampuni ni kuwezesha wafanyabiashara wa kitanzania kupata fursa ya masoko ya nje,” alisema na kuwataka Watanzania wenye vikundi vya ujasiriamali, kampuni, taasisi za umma na binafsi kushiriki kwenye maonesho hayo kwa kuwa ni Jukwaa muhimu sana la kukutana wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali za maarifa ya kisasa ya uzalishaji, ufungashaji na usambazaji wa bidhaa kupata soko la ndani na nje pamoja na ajira.