Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAAFISA wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoani Tabora wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya kuomba rushwa kwa wananchi ili kuwasaidia kupata vitambulisho hivyo.
Wakizungumza kwa uchungu katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Tabora, baadhi ya madiwani wameoneshwa kukerwa na tabia ya Maafisa hao na kutaka hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi yao.
Diwani wa kata ya Tambuka-reli Zinduna Kisamba alisema watumishi hao wamekuwa wakiwatolea lugha zisizo na staha wananchi wakati wa kutekeleza zoezi la uandikishwaji kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.
Alisema kitendo hicho kimefanya zoezi hilo kusuasua katika maeneo mengi ndani ya manispaa hiyo hali inayopelekea kukwamishwa zoezi hilo na wale walioaminiwa na serikali kutoa huduma hiyo kutoaminiwa tena na jamii.
Alibainisha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakikosa huduma za msingi kwa kukosa namba za NIDA jambo ambalo limepelekea kuwepo malalamiko mengi miongoni mwa jamii kutokana na utendaji mbovu wa Maafisa hao.
Naye diwani wa kata ya Ikomwa, Salum Msamazi alisema licha ya kufuata huduma hiyo katika ofisi za NIDA bado wamekuwa wakitolewa maneno machafu na wengine kuombwa pesa ili kupata huduma hiyo tofauti na maelekezo ya serikali ya huduma hiyo kutolewa bure kwa Watanzania wote.
Mstahiki Meya wa manispaa hiyo Ramadhan Kapera alimwagiza Meneja wa NIDA Mkoani humo kuwachukulia hatua wale wote wanaokwamisha zoezi hilo kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ikiwemo kutumia lugha za maudhi.
Alieleza kuwa vitendo hivyo havikubaliki kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuona kila mtanzania mwenye sifa anapata kitambulisho hicho bila gharama yoyote na sio kutumia nyadhifa zao kunyanyasa wananchi.
Akijibu hoja hizo Meneja wa NIDA Mkoani hapa Issakwisa Mwampulo alikiri kupata malalamiko ya vitendo hivyo na kubainisha kuwa wameanza kuchukua hatua kwa Maafisa wote waliolalamikiwa kujihusisha na vitendo hivyo.
‘Tayari tumewasimamisha kazi baadhi ya Maafisa waliotajwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na kutumia lugha zisizo na staha kwa wananchi, vitendo hivyo havikubaliki na ni kinyume na maadili ya kazi yao’, alisema Mwampulo.
Alifafanua kuwa kwa sasa wameweka utaratibu mzuri utakaowezesha wale wote ambao hawajapata kujiandikisha ili kupatiwa vitambulisho hivyo.
Mwampulo aliongeza kuwa hakuna kitambulisho chochote kinachotolewa kwa kutoa rushwa au kwa siku moja, wananchi wanatakiwa kufuata taratibu na kuwa na taarifa zao sahihi ili kurahisisha zoezi hilo.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu