January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Manispaa ya Bukoba yashughulikia mashauri 92 ya ukatili wa watoto

Na Ashura Jumapili,Bukoba,

Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kwa kushirikiana na wadau wa mapamabano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa watoto wameweza kushughulikia na kutatua mashauri mbalimbali ya watoto yapatayo 92 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi juni mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Bukoba Wanchoke Chinchibera katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 16,mwezi Juni yaliyofanika katika viwanja vya Mayunga mjini Bukoba.

Chinchibera ,amesema watoto waliofanyiwa ukatili wa kihisia ni 54 wakike 43 na wakiume 11,ukatili wa kiuchumi watoto kufanyishwa kazi 34 kati yao wavulana 30 na wasichana nne,ukatili wa kingono kwa watoto tatu wa kike na tukio moja la ukatili wa kimwili kwa mtoto wa kike.

Amesema katika mashauri hayo 92 ya ukatili na unyanyasaji wa watoto mashauri yaliyofikishwa mahakamani ni 38 .

Amesema lengo la manispaa ya Bukoba ni kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaisha na kuhakikisha watoto wanapata haki zao ikiwemo fursa za kupata elimu na kutokomeza utumikishwaji wa watoto katika shughuli za kiuchumi.

Amesema watoto wamepewa elimu ya stadi za maisha,Afya ya uzazi ,hedhi salama pamoja na athari ya mimba za utotoni kwa wanafunzi 2,485.

Amesema kauli mbiu ya mwaka huu”Tuimarishe ulinzi wa mtoto kutokomeza ukatili dhidi yake jiandae kuhesabiwa”inawakumbusha wasimamizi wa sera na sheria,wazazi ,walezi ,serikali na wadau wengine kuhusu wajibu wao wa kuendelea kulinda,kusimamia na kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto.

Naye mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Gibson Godson,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alisema wanapinga ubaguzi wa kielimu hivyo hakuna mtoto ambaye haendi shule katika eneo lake asilimia 99 ya watoto wamekwenda shule.

Godson,amesema siku ya mtoto wa Afrika ni chimbuko la azimio lililopitishwa na viongozi wa umoja wa nchi huru mwaka 1990 ili kukumbuka watoto zaidi ya 2000 waliopoteza maisha na wengine 1000 kujeruhiwa huko Kitongoji cha Soweto nchini Afrika kusini wakati wakidai haki zao ikiwemo kupinga elimu ya ubaguzi mwaka 1976.

Amesema katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi amemuagiza mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba na Afisa elimu kupata taarifa za mashirika na idadi ya watoto wanaohudumiwa na mashirika hayo ili watoto wasiohudumiwa serikali ione namna ya kuwasaidia kupata haki zao za msingi.

Hata hivyo amemuagiza afisa elimu kushirikiana na wakuu wa shule wote katika manispaa ya bukoba kupanda matunda ya parachichi miche 50 kila shule ili watoto waweze kupata matunda wakiwa shuleni.

Rehema jonn (14)amesema jamii ya kitanzania imekuwa na kasumba ya kuwafungiwa watoto wenye ulemavu majumbani na kuwanyima haki yao ya kusoma na kucheza na wenzao.

Amesema watoto hao wana haki ya kusoma ,kuabudu na wakifichwa wanajiona kutengwa.

Amesema elimu mwangaza kwa Watoto wakikosa elimu wamekosa mwangaza.