November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mamilioni ya Rais Samia utambulisho mpya michezoni 

Na Philemon Muhanuzi,TimesmajiraOnline,Dar

MABUNDA ya pesa yamezoeleka kuonekana katika kipindi hiki yakiwa mkononi mwa  wasaidizi wa Rais Samia tayari kuwapa manahodha wa Yanga na Simba kila wanaposhinda mechi zao. 

Msemaji wa serikali Gerson Msigwa anapiga picha za video akitamba namna pesa hizo zinavyowafikia manahodha mara tu baada ya mechi kuwa zimemalizika wakati wachezaji bado wakiwa na miili iliyolowa jasho. 

Likifungwa goli moja nahodha anao uhakika wa kupokea shilingi milioni tano. Timu ikishinda mechi nahodha anao uhakika wa kulipwa shilingi milioni kumi.

Wale wanaharakati wenye sifa za kuandika malalamiko na kejeli mitandaoni hawajabaki nyuma hata kidogo.  

Wanakuja na kauli kwamba wakati mamilioni yanagawiwa kwa Simba na Yanga kwa kupata ushindi wa mechi za hatua ya makundi na robo fainali ya ligi ya mabingwa zipo shida nyingi zenye kuhitaji utatuzi wa kiserikali mpaka kufikia kupokea misaada ya fedha za wafadhili!. 

Rais Samia angeamua tu kutoonyesha kuguswa na mchezo wa soka hao hao wanaharakati wangekuja na maandiko yao yenye kuiponda serikali yake kwa kuwa mbali na michezo. 

Wapo wenye fikra kwamba aliyenacho huongezewa na hawaoni ni kwanini fedha hizi wanazopewa manahodha wa vilabu vya Simba na Yanga zisishuke chini zaidi na kuigusa michezo kwa mapana yake. 

Katika kipindi cha miaka mitatu ya urais wa Samia Suluhu Hassan mengi yalitegemewa kuonekana yakikwama na kudorora lakini uhalisia umekuwa na majibu ambayo ni kinyume kabisa. 

Labda ni kwa sababu michezo ilikuwa na misingi iliyoendelea kuwekwa kuanzia awamu ya nne. 

Rais Samia anajikuta akiserereka na masuala mengi aliyoyakuta yameanzishwa tayari. 

Hajakubaliana na kuona kuwa kile kilichoanzishwa na marais waliomtangulia kinakuja kufa kifo cha kawaida katika awamu ya sita. 

Ameamua kuuendeleza moto ule ule wa watangulizi wake. Pia amekuja na Baraka zake binafsi akiwa Amiri Jeshi Mkuu. 

Hakuna mwenye akili timamu na aliyefikisha umri wa zaidi ya miaka arobaini asiyeshangazwa na hatua walizopiga Yanga na Simba haswa kimataifa. 

Miaka na miaka wimbo umekuwa ni ule ule wa siku zote. Kwamba mwaka 1975 ndio Simba ilishiriki kwa mara ya mwisho mechi ya nusu fainali ya klabu bingwa afrika {wakati huo ikiitwa hivyo}. 

Ni miaka 49 iliyopita na siku zikiendelea kwenda kasi. Hatimaye ndani ya awamu ya sita tunaziona timu hizi mbili zikizaliwa upya kabisa. 

Kuanzia juu katika uongozi mpaka muitikio mzima wa huku kwenye ushabiki wa majukwaani. 

Mapinduzi haya ya uendeshaji wa mpira wetu wana chanzo ambacho ni muitikio chanya wa kiserikali kwa maana ya kuwa na utayari wa kutoa ushirikiano pale inapobidi. 

Sio kazi nyepesi kwa Yanga kuwa na wazee wenye ushawishi mpana wa kualika wafanyabiashara pasipo uwepo wa ushirikiano na serikali ya awamu ya sita. 

Wanaotoa pesa nyingi kiasi cha Yanga kuweza kuleta wachezaji wa viwango vya Pacome Zouzoua, Khalid Aucho na Djigui Diarra wanafanya hivyo baada ya uwepo wa mazingira ya maelewano baina yao na uongozi wa juu kabisa wa awamu ya sita. 

Hata huko Simba ambapo michakato ya mabadiliko ilianza tangu awamu ya tano pia kuna ushirikiano chanya kati ya uongozi wa timu na ule wa kiserikali. 

Mpaka inapigwa picha ya Msigwa akiwapa mabunda ya noti manahodha wa Yanga na Simba kunakuwa na mengi yaliyo chanya yanayofanyika mbali na macho ya watu. 

Ombi lililo maalum kabisa na kwa serikali ya awamu ya sita kutoishia kwenye kutoa malipo mengi kwenye mpira wa miguu pekee. 

Kuna haja ya kuitazama kwa kina michezo mingine na kupima ushiriki wetu kwa ujumla. 

Huko kwa majirani zetu Uganda wameweza kuingiza ratiba ya michezo kwenye shule za sekondari na taasisi mbalimbali zinazotoa elimu. 

Kila mwaka kuna uhakika wa uwepo wa michezo mingi na waalimu wanakuwa na urahisi wa kugundua vipaji vipya na kusimamia ukuaji wa vijana hao. 

Kuna suala la maandalizi ya michuano ya AFCON mwaka 2027 huu na uwe ni muda muafaka ya serikali ya awamu ya sita kuvitazama kwa ukaribu viwanja vyote vinavyotumika hapa nchini mbali ya vile vitakavyojengwa kuelekea kufanyika kwa michuano hiyo. 

Ni muda wa utaalam wa ujenzi na utunzaji wa viwanja kupewa kipaumbele cha makusudi katika bajeti nzima za serikali ya awamu ya sita kuelekea mwaka huu utakaokuwa ni maalum kwa Tanzania. 

Bravo Rais Samia umekuwa ni kiongozi uliyeweza kuwanyamazisha wote wenye kuishi na zile dhana za mfumo dume vichwani mwao. 

Wale ambao hawakutegemea hata siku moja nchi inayoitwa Tanzania kuja kuongozwa na Rais wa jinsia isiyokuwa ya kiume wanajikuta wakikosoa mengi kwa sababu ya chuki zaidi kuliko kuwa na mizania ya uhalisia. 

Na mengi yanaendelea kufanyika kwa kufuata ratiba zenye kujulikana kwa miaka kadhaa bila ya lolote kuonekana kuharibikia njiani. 

Tunaziombea kwa Mungu Yanga na Simba ziweze kuwatoa wapinzani wao katika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa. 

Mabilioni ya Rais Samia yatawasubiri manahodha wa timu hizi iwapo zitapata ushindi haswa baada ya mechi ngumu sana kumalizika viwanjani.