November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mama Zainabu: Tuwasaidie wakina mama katika kufanikisha maendeleo ya jamii

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib, amesema Jamii inapaswa kuwasomesha watoto kwa malengo ya kupambana na soko la ajira ikiwemo kujiajiri hapo baadae.

Mama Zainab ameyasema hayo leo Aprili 19, huko Mtambwe Kivumoni, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, akiongea na wajasiriamali Wanawake katika kuangalia namna bora ya kupambana na changamoto za kimaisha zinazowakabili kila siku.

Mama Zainab ametoa ufafanuzi na kuelezea mbinu mbali mbali zitakazowasaidia wanawake katika kuzilea familia na jamii kwa ujumla ikiwemo kuwajengea mazingira mazuri ya kimasomo watoto wao.

“Tunahitaji kukijenga kizazi chetu katika kupata elimu ambayo itawakomboa kimaisha na kuweza kujiajiri, kwani ongezeko la uhitaji wa ajira za Serikali ni kubwa”, amesisitiza Mama Zainab.

Nao Wanakijiji pamoja na viongozi wa vikundi hivyo vya ujasiriamali vya wanawake, wameeleza changamoto zao ikiwemo mitaji na vitendea kazi sambamba na kuomba ushirikiano wa Serikali katika kuzitatua.

Katika ziara yake hiyo Mama Zainab amepata fursa ya kukagua miradi ya wanakijiji kama Ufugaji, Kilimo na shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na kina mama kama ni sehemu ya Ujasiriamali, katika vijiji vya Kisiwani kwa Binti Abeid, Wete Limbani, Kipangani na Selemu kutoka mkoa wa Kaskazini Pemba.