February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mama Maria Nyerere aitaka CCM kudumisha uwezo wa Taifa kujitegemea

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

MJANE wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, ameitaka CCM kuendelea kutimiza wajibu wake wa kuzisimamia Serikali zake zote mbili, ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uwezo wa kujitegemea, hasa katika kujilisha.

Mama Maria alisema hayo alipokutana na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyefika nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Msasani, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kumsabahi na kumjulia hali, mapema jana Februari 20, 2025.

Aidha ameitaka CCM kuendelea kusimamia sera yake, huku akisema kuwa, uhuru wa Taifa lolote unakamilima pale linapokuwa na uwezo wa kujitegemea.

“Naomba tu muendelee kusimamia sera ya msingi ya CCM kuhusu kujitegemea… Uhuru wa taifa unakamilika zaidi pale taifa linapojitegemea, hasa katika kujilisha na kuwa na chakula. CCM isiache wajibu wake wa kuzisimamia serikali zake zote mbili ili nchi yetu iendelee kujitegemea,” alisema Mama Maria.