January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mama adaiwa kumuua mwanawe ili apate kazi

Na Steven Augustino,TimesMajira Online,Tunduru

MWANAMKE wa miaka 24 mkazi wa kijiji cha mwenge katika kata ya Mtina Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma aliyetambulika kwa jina la Neema Athumani Chama anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake.

Taarifa zinaeleza kuwa mwanamke huyo alitekeleza mauaji hayo Desemba 24,mwaka huu, baada ya kumpatia sumu ya Panya mtoto wake wa kiume aliyetambulika kwa jina la Rashfod Tariq (4) baada ya kumuwekea sumu hiyo kwenye soda.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kutekeleza unyama huo alichimba shimo na kwenda kumzika peke yake na baadae kutoroka kijiji hapo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo mtuhumiwa alikamatwa akiwa safarini kuelekea mkoani Arusha alikodai kuwa alikuwa anakwenda kwa ajili ya kufanya kazi za dani kutokana na ugumu wa maisha baada ya mzazi mwenzake kumtelekeza na kukataa kuhudumia mtoto.

Akiongea na gazeti hili akiwa chini ya ulinzi wa Polisi mtuhumiwa huyo amekiri kufanya tukio hilo baada ya kupewa masharti na mwajiri wake wa mkoani Arusha kuwa kama anahitaji kazi aende bila mtoto.

“Nilimuwekea sumu ya panya kwenye soda ili afe na mimi nipate nafasi ya kwenda kutafuta maisha mkoani Arusha bada ya mzazi mwenzangu kunitelekeza na mtoto tangu akiwa mdogo na kila ninapo mwambia aje amchukue mtoto wake amekuwa akikataa” amesisitiza Neema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa amedhibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba Polisi bado wanaendelea na uchunguzi juu ya chanzo cha tukio hilo.

Aidha Kamanda Maigwa aliendelea kueleza kuwa mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa taratibu za mahojiano ya awali.