Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
MALI zote zinazomilikiwa na Vyama vya Ushirika vya Wakulima (Amcos) Mkoani Tabora zimetambuliwa na kuthaminiwa ili kujua thamani halisi ya mali za kila chama ikiwemo ofisi, samani za ofisi, idadi ya mashamba na vifaa vinginevyo.
Hayo yamebainishwa jana na Afisa Mthamini wa Mali za Vyama vya Ushirika (Amcos) Ismail Chingwele alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya hatua ambazo zimechukuliwa na Ofisi ya Mrajisi katika kuimarisha vyama hivyo.
Amesema kuwa zoezi hilo linalofanywa na Kampuni yao ya CPM Land Developers Ltd ya Jijini Dar es salaam limewezesha kutambuliwa kwa vyama vya wakulima 497 na kati ya vyama hivyo 140 vimefanyiwa uthamini wa mali zao mwaka huu.
Amebainisha kuwa zoezi hilo litafanyika katika Mkoa mzima na katika kila Wilaya hadi sasa wamethaminisha mali za vyama vilivyooneshwa kwenye mabano, Kaliua (20), Uyui (27), Urambo (17), Sikonge (24) na Manispaa (7).
Chingwele amefafanua kuwa kabla ya kuanza uthaminishaji wa mali za Amcos hizo ilibainika kuwa zilikuwa na thamani ya sh bil 19.8 lakini baada ya uthaminishaji kulingana na thamani ya soko mwaka huu vina mali zenye thamani ya sh bil 34.6.
Kwa vyama hivyo 140 ametaja mali zilizotambuliwa na kuthaminiwa kuwa ni ardhi yenye ukubwa wa ekari 198 ambayo ina thamani ya sh mil 35.6, majengo ya ofisi 97 yenye thamani ya sh bil 2.3 na maghala 153 yenye thamani ya sh bil 15.8.
Mali nyingine ni samani za ofisi zipatazo 12,077 zenye thamani ya sh mil 300, vifaa vya uchapishaji ofisini vipatavyo 1,160 vyenye thamani ya sh mil 7.8.
Nyingine ni zana za mitambo ambazo ni jenereta 3, mitambo 3 ya kuchakata nafaka, mtambo 1 wa kuvutia maji, mizani ya analojia 278 na kidijitali 192 yenye thamani ya sh mil 388.1.
Ametaja mali nyingine kuwa ni vyombo vya moto na mashine ambavyo ni gari 1 la kutembelea, magari 37 ya kubebea mizigo ya wakulima, pikipiki 15 na matrekta 13 vyote vikiwa na thamani ya sh mil 911.
Chingwele amebainisha vifaa vya TEHAMA kuwa ni komputa mpakato (laptop) 112, komputa kubwa za mezani (desktop) 17, printa 13 na mashine za kudurufu karatasi (photocopier) 7 vyote vikiwa na thamani ya sh mil 98.9.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani hapa Venance Msafiri amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu na watahakikisha mali za Amcos zote zinatambuliwa na kuthaminiwa ili kuepusha ubadhirifu ndani ya vyama hivyo.
Amewataka Viongozi wa Amcos zote kutoa ushirikiano kwa Kampuni hiyo ili kuhakikisha mali zao zinatambuliwa na kuthaminiwa ili kuchochea soko zuri la mazao yao na kukopesheka kirahisi na taasisi za kifedha.
Mwisho
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa