Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline, Dar
KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amekemea kasumba inayoendelea ya kutaka kumtofautisha Rais Samia Suluhu Hassan na mtangulizi wake, hayati John Magufuli.
Makonda alikemea hayo wakati wa hafla ya kupokea ndege mpya ya abiria Boeing B737-9 Max ambayo imetengenezwa nchini Marekani.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege hiyo.
“Huwezi kuwatenganisha hawa (Samia na Magufuli) watu na viongozi wengi wanafiki, wanaotafuta kujipendekeza kwa Rais Samia kila wakipata jukwaa wanataka kumfanya Samia kama si sehemu ya Dkt. Magufuli,” amesema Makonda na kuongeza;
“Kama msemaji wa chama kila anachokifanya Rais Samia, ndicho alikifanya Magufuli. Walisimama wakazunguka katika nchi hii kutafuta kura huwezi kuwatenganisha na waziri Mkuu wao yule pale Kassim Majaliwa.
Ningetamani leo (jana) iwe siku ya mwisho ya unafiki wa viongozi na wanasiasa uchwara wanaopambana kuwatenganisha viongozi hawa.”
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,Profesa Godius Kahyarara, alisema watendaji wa wizara hiyo wana jukumu kubwa la kusimamia ndege zinazonunuliwa na Serikali ili kuunga mkono jitihada za uwekezaji zinazofanyika.
Prof. Kahyarara ameihakikishia Serikali kuongezeka kwa ndege hizo kutaongeza mtandao wa shirika la hilo la ndege na kuongezeka kwa biashara wanayoifanya.
“Niwahakikishie tuna jukumu kubwa la kusimamia ndege zinazonunuliwa na Serikali na mpaka sasa tumeona mafanikio makubwa kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kufanya uwekezaji katika shirika hili,”alisema .
“Nikuhakikishie Waziri Mkuu kazi wanayofanya wana uwezo wa kujilipa mishahara, kununua mafuta ya ndege na uwezo wa kufanya matengenezo kwa hiyo nina imani jinsi ndege zinavyoongezeka zitaendelea kutoa mchango mkubwa,”alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema Serikali imetumia gharama kubwa kununua ndege ili Watanzania waweze kufaidika.
“Mtaji mkubwa wa ndege hizi ni amani. Sisi na wenzangu tumedhamiria kulinda amani ya Mkoa wa Dar es Salaam na mtu yeyote ambaye yuko tayari kutishia na kuvuruga amani ya mkoa huu tutamvuruga hata kabla ya kutoka kwenye geti,”amesema Chalamila.
More Stories
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto