Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Geita
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wakazi wa Kata ya Katoro mkoani Geita kutoa ushirikiano katika ngazi ya Vijiji, Kata, Wilaya mpaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuwa wanaofanya uhalifu katika ukanda huo wanapatikana na kuchukuliwa hatua stahiki.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Paul Makonda mapema leo akiwa katika Kata ya Katoro, wilayani Geita, Mkoa wa Geita ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Kanda ya ziwa.
Makonda amesema kwa kufanya hivyo itasaidia Katoro na wilaya yote kubaki kuwa sehemu ya utulivu, amani na mshikamano kwa wananchi kufanya shughuli za maendeleo.
“Eneo hili la Katoro lina matukio ya uhalifu na inawezekana tunawafahamu wahalifu, Chama kingetamani kuona mnatoa ushirikiano mzuri kuanzia ngazi ya Vijiji , Kata, Wilaya, na kwa Mkuu wa Mkoa ilii wanaochafua ukanda huo kwa uhalifu wanabainika na kuchukuliwa hatua ili Katoro na Busanda na wilaya nzima ya Geita na mkoa wetu ubaki kuwa ni sehemu ya utulivu, amani na mshikamano kwa wananchi kufanya shughuli za maendeleo” Alisema Makonda
Kuhusu changamoto kubwa ya maji katika Kata ya Katoro, Makonda amewasiliana na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ili kujua ni hatua gani zinachukuliwa kuondokana na changamoto hiyo.
Akijibu swali la Makonda, Aweso amesema katika Kata hiyo kuna mradi wa shilingi bilioni 6 ambapo kwa sasa upo katika hatua ya mwisho, hivyo ameomba wiki 3 kukamilisha mradi huo ili wananchi wa Kata hiyo wapate maji safi na salama.
“Mradi huo wa shilingi bilioni 6 umefika asilimia 92 na Mbunge wa jimbo hilo alikuja kuniomba shilingi milioni 500 na tumeshaidhinisha, mradi huo naomba wiki 3, wanakatoro Buseresere watakunywa maji safi na salama” amesema Waziri wa Maji, Juma Aweso.
“Kama Wizara tumepewa maeneo mahususi hasa Kanda ya Ziwa, ambapo Ziwa Victoria lazima litumike kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji mkoani Geita na maeneo yote ya Kanda ya Ziwa ili kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji katika miji 28, Geita mjini tuna asilimia 75, amnbapo kwa sasa kuna mradi mkubwa wa zaidi Dola Milioni 500 kwa eneo la Geita mjini na tumepewa zaidi ya Bilioni 128 na mkandarasi yupo site” amesema
Aweso amesema Mkoa wa Geita una Vijiji 489, ambapo kati ya vijiji hivyo 333 vimeshafikiwa maji , hivyo kazi waliyopewa na Rais Samia ni kuhakikisha vijiji vyote vinapata maji safi na salama na kwamba Serikali imetoa zaidi ya Bilioni 20 vijijini kuhakikisha miradi ya maji inajengwa katika maeneo mbalimbali.
Akiendelea kutoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji maji, Aweso amesema “Rais Samia ametununulia mitambo 25 ya uchumbaji visima ambapo eneo ambalo linahitaji kuchimbwa kisima lazima tukachimbe na watu wapate huduma ya maji safi na salama,
“Pia Rais Samia ametununulia mitambo ya uchimbaji mabwawa seti 5 na ambapo kila eneo linalohitaji bwawa tutachimba kuhakikisha watu wanapata maji safi na salama”
Aweso amesea watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani inatimia.
Mbali na hayo, Makonda ametaka ufafanuzi kuhusu changamoto ya Barabara za TARURA Katoro na Buseresere ambapo Meneja wa TARURA Kata ya Katoro Mhandisi Thereza Bernado Kata hiyo amesema “Ni kweli Kata ya Katoro na Buseresere kuna changamoto ya barabara ambayo inachangiwa na idadi kubwa ya watu ambapo idadi ya kilometa za barabara, Katoro pekee ni Km 153.’
Katika ya Kilometa hizo kuna kilometa 2.4 za lami ambazo zimetekelezwa kupitia fedha tulizopewa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2022 kwaajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, “ ameongeza Meneja wa TARURA, Mhandisi Thereza
“Kwa mwaka huu tuna barabara tunazokwenda kutekeleza Katoro kwa shilingi Milioni 647 ambazo ni kutoka Duka la Dawa kwenda Bulenga (Km 3) , Polisi hadi Buseresere (Km 1.2), Stendi kwenda Shule ya Msingi Ludete (Km 1.5), barabara ya Ushirombo (Km 1.2), mitaro Km 1/½, lami mita 250 kuelekea hospitali “
Amesema bado zinahitajika fedha ili kukamilisha miradi hiyo na wanaendelea kufanya tathmini ikiwemo barabara inavyokwenda hospitali ili ikamilike ambayo Ina km 6 na sasa wameshatekeleza mita 800 katika km hizo.
Matukio Mbalimbali katika picha
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi