Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Iringa
Makandarasi wameaswa kuandaa zabuni shindani na nzuri kwa kuzingatia misingi ya utayarishaji wa zabuni ikiwa ni pamoja na uandaaji wa bei za zabuni. Aidha, wameaswa kutumia ujuzi walioongeza katika kuboresha zabuni na pia kuendelea kutafuta na kuongeza ujuzi na maarifa kupitia njia mbalimbali kama mafunzo rasmi, mitandao, mikutano, n.k.
Akizungumza wakati wakufunga mafunzo ya Maandalizi ya Zabuni (Construction Pre – Contract Practices) yaliyofanyika kwa siku tatu mkoani Iringa, Msajili msaidizi wa CRB, Mhandisi. David Jere, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kukuza ujuzi kwa makandarasi pamoja na waajiri kuhusiana na namna nzuri ya maandalizi ya zabuni.
“Kupitia mafunzo haya wamejifunza mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji ikiwemo kuhakikisha maandalizi ya zabuni shindani ambazo Makandarasi watapata thamani ya kazi watakazofanya (Value for the Workdone) lakini pia mwajiri apate thamani ya fedha atakazolipa kwa kazi iliyofanywa (Value for money)”, alisema Mhandisi. Jere.
Sambamba na hayo aliwaomba waajiri wa Makandarasi kuwa miradi iandaliwe vizuri, ikiwemo nyaraka za zabuni zenye taarifa zinazojitosheleza ili kuwawezesha wazabuni kuelewa vizuri matakwa ya mwajiri katika utekelezaji wa miradi husika ili kuleta tija katika utekelezaji wa miradi na kuliletea Taifa letu maendeleo zaidi.
“Pande zote zinazohusika na utekelezaji wa miradi ambao kwa Makandarasi unaanzia katika hatua ya maandalizi ya zabuni, kutimiza wajibu na haki kama ilivyoanishwa katika mikataba husika”, alisema Mhandisi Jere.
Pamoja na hayo alisisitiza kuwa makandarasi washiriki mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na CRB ili kuwaongezea thamani kwasababu ujuzi huwa unaongeza ufanisi katika shughuli yoyote ile na wafanye kwa vitendo yale yote waliyofundishwa, kushirikiana na kutimiza wajibu wao katika miradi mbalimbali na kuwa wafanyabiashara wa kweli na halali bila kukwepa kulipa kodi, kughushi nyaraka na kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria za nchi.
Kwa upande wake kama mshiriki, Mhandisi Yahya Mnali, alisema amefurahishwa na mafunzo hayo kwakuwa yanawafanya kujiamini katika biashara ya ukandarasi kuanzia uombaji wa zabuni na utekelezaji wa miradi.
“Kupitia mafunzo haya tumejifunza kwa vitendo mbinu na kanuni za uandaaji wa zabuni kuanzia uombaji na tulishindanishwa maana tuliandaa makampuni ya muda ambapo tuliandaa mchakato wote kuanzia uchujaji mpaka kumpata mshindi, kitendo hiki kimetuimaimarisha zaidi na kunoa zaidi katika kuandaa zabuni.”, alisema Mhandisi Mnali.
Aidha, alitoa wito kwa Makandarasi wengine amabao hawajawahi kufanya mafunzo yanayoandaliwa na CRB kujitokeza, kujifunza katika kuijiongezea ujuzi utakao wasaidia kufanya kazi zao kwa urahisi na ubora.
Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa 12 hapa nchini wakiwemo Makandarasi na Waajiri.
More Stories
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo
TAKUKURU,yasaidia kurejesha hekali 8