Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Sabasaba Mkoani Njombe. tarehe 02 Aprili, 2022 Aidha wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani pamoja na watanzania wote wameombwa kushiriki kwenye uzinduzi huo.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge kwa mwaka 2022 ni “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa”.
Akiongea na waandishi wa habari leo, tarehe 29 Machi, 2022, Jijini Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, amefafanua kuwa pamoja na Kauli Mbiu hiyo, Mbio hizo zitaendelea kuelimisha na kuihamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa Lishe bora, Mapambano dhidi ya Rushwa, Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, Mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na Mapambano dhidi ya Malaria.
Katambi amefafanua kuwa, baada ya Uzinduzi huo, Vijana sita walioandaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, watakabidhiwa jukumu la kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Mikoa 31 na Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195. Ameongeza kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza shughuli za maendeleo.
“Mwenge ni jicho la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, katika maeneo ambayo kote ana vyombo, anatawala na anamifumo ya kiserikali, hilo ni jicho la ziada, kote unakopita unakagua shughuli za maendeleo na unamulika miradi kwa kuangalia fedha zimetumika kama zilivyo pangwa na kama haijatekelezwa ipasavyo hatua stahikli zinachukuliwa” Mhe. Katambi
Amefafanua kuwa, Mwenge wa Uhuru na Mbio zake umeendelea kuwa muhimu kwa taifa kwa kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi za kisiasa, dini wala makabila. Aidha, amebainisha kuwa, Falsafa ya Mwenge wa Uhuru, ndio chimbuko la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964 na Azmio la Arusha la mwaka 1967.
Katambi , amesisitiza kwa upande wa Kimataifa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana yake ya kumulika hata nje ya mipaka yetu kwani Tanzania imeendelea kuhamasisha amani ndani ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Jangwa la Sahara na Afrika na Duniani kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwa msuluhishi wa amani Afrika na imeshiriki katika ukombozi wa Bara la Afrika.
Mwenge wa Uhuru ambao kwa mwaka huu utaanza Mbio zake Mkoani Njombe tarehe 02 Aprili, 2022 unatarajiwa kufikia Kilele chake Mkoani Kagera tarehe 14 Oktoba, 2022. Mwenge huo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961.
More Stories
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo