Na Penina Malundo,Timesmajira,Online
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan leo amezindua Mradi wa Usambazaji wa Maji Kutoka Kisarawe-Pugu-Gongolamboto na maeneo ya jirani wenye thamani ya Shilingi bilioni 6.9.
Pia ameipongeza Mamlaka ya Maji jijini Dar es Salaam,DAWASA kwa jitihada kubwa wanazofanya kusogeza huduma ya Maji kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Shule ya Sekondari Pugu,wakati akiongea na wananchi,wanafunzi wa Shule hiyo,Walimu na wafanyakazi wa Dawasa amewataka Wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya Maji na kulipa Bili za Maji kwa wakati.
Aidha Mama Samia amesema kama DAWASA itaendelea na kasi hiyo ana matumaini makubwa kuwa ifikapo 2025 kilio Cha uhaba wa Maji Dar es salaam kitabaki kuwa historia ambapo kwa mujibu wa DAWASA hadi kufikia sasa upatikanaji wa maji Jijini humo upo kwa asilimia 92.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Juma Aweso amesema taswira ya wizara ya maji miaka ya nyuma ilikuwa mbaya miradi ilikuwa ikijengwa na kutoa maji wiki mbili na baada ya muda hayatoki.
Amsema wamewatumia wataalamu wao wa ndani katika maeneo ya vijijini ambayo yana tatizo kubwa la maji na wametekeleza miradi ya maji 192 ambayo gharama za yake ilikuwa Sh bilioni 207 lakini wametumia Sh bilioni 163 na kuokoa bilioni 44.
“Leo ukienda Sumbawanga vijijini mradi ambao ulitakiwa kutekelezwa kwa Sh bilioni 6.7 wa vijiji 10 tumeweza kutekeleza kwa Sh bilioni 1.5 na wananchi wa vijiji vitano wanapata huduma ya maji leo ukienda Makete mradi wa vijiji saba bilioni 6 tumeitejekeza kwa Sh bilioni 1.5 na wananchi wanapata maji nataka niwaambie wakandarasi na wataalamu wa Wizara ya Maji vipo vya kuchezea na ukishiba chezea kidevu ama kitambi chako sio miradi ya maji tutakushughukikia,” amesema
Aidha ameipongeza Dawasa kwa kupiga hatua katika ukusanyaji wa fedha hadi kufikia Sh bilioni 13 kutoka Sh bilioni 7.5.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam , Aboubakar Kunenge amesema mkoa umejipanga vizuri kuhakikisha unasimamia kikamilifu Miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Jijini humo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Ameipongeza DAWASA kwa kuweza kujiendesha Jambo linalopelekea miradi mingi kwa Sasa kutekelezwa kwa fedha za ndani kitendo kinachoonyesha Mamlaka hiyo imedhamiria kufanya mageuzi kwenye suala la upatikanaji wa maji Safi na Salama.
Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema tangu Serikali ya awamu ya Tano iingie Madarakani wamefanikiwa kutekeleza miradi ya Maji Dar es salaam yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja.
Hata hivyo amesema Mradi huo wa Pugu itawezesha kufikisha huduma ya maji kwa wakazi wa Gongolamboto, Chanika, Zingiziwa, Banana, Ukonga, Segerea na maeneo yote ya jirani.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam