- NMB yakabidhi vifyaa vya kuezekea madarasa vya Mil. 22/-
Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amezindua huduma ya mikopo nafuu ya Boti za Kisasa za Uvuvi na vifaa vyake inayotolewa na Benki ya NMB ‘NMB MastaBoti,’ huku akiitaja taasisi hiyo kuwa msaidizi mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), katika kukuza Uchumi wa Buluu na kuwaletea mandeleoz endelevu wananchi.
Makamu wa Rais SMZ aliyasema hayo Jumanne Januari 9, katika Viwanja vya Skuli ya Msingi ya Tasini, iliyopo Kiwani Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar, wakati akizindua NMB MastaBoti, sambamba na kupokea boti tano za mkopo na vifaa vyake, zikiwa zimekatiwa bima, zilizotolewa na benki hiyo kwa Jumuiya ya Wavuvi Kiwani (Juwaki)
Sambamba na uzinduzi na makabidhiano ya boti hizo, Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, alimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais msaada wa vifaa vya kuezekea vyumba vya madarasa ya skuli tatu za Chambani, Kondeani na Nanguji, zilizopo Kiwani, ambavyo ni mabati 400, mbao na misumari, vyenye thamani ya Sh. Milioni 22.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais aliipongeza NMB kwa kusikiliza maombi ya Wana Kiwani na kuyafanyia kazi kwa haraka, huku akibainisha kwamba boti za kisasa ilizokabidhi kwa Juwaki, zinaakisi na kusapoti dhamira na Sera ya Uchumi wa Buluu inayotekelezwa na SMZ chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.
“NMB imejipambanua kuwa ni moja ya benki kubwa Afrika, na SMZ inajivunia ushirikiano uliopo baina yetu na taasisi hii, ambayo imetusaidia sana katika maeneo mbalimbali. Tunaishukuru sana kwa namna inavyowatendea haki Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla, kwa sababu kila eneo, kila sekta Serikali ilikopiga hatua, benki hii imekuwa nyuma yetu.
“Leo wamekuja hapa kutimiza maombi yetu Wana Kiwani ambayo niliyatoa kwao ya kutukopesha vifaa vya kisasa vya uvuvi, kwani Serikali yetu inataka kuwafanya wananchi wa hapa wanakuwa ‘busy’ kwa shughuli za kimaendeleo. Boti hizi tano zinaenda kuwaweka ‘busy’ wavuni 20, ambao nyuma yao kuna mnyororo mpana wa wasaidizi wa shughuli zao,” alibainisha.
Aliwataka Juwaki kuhakikisha wanazitumia vema boti hizo kwa kurejesha kwa wakati ili kutoa fursa ya wakopaji wengine kufikiwa na huduma hiyo, na kuwataka kutojiuliza soko la bidhaa za uvuvi, kwani hilo ni jukumu la Serikali ambayo inapambana kuweka mazingira bora, huku akiwaahidi kuwanunulia mafuta ya kuanzia kazi kwa boti zote (lita 30 kila moja).
“Naamini hamtoniangusha na hapa niwahakikishie NMB, kwamba Juwaki na wanachama wao wameniahidi kuwa watalipa marejesho ya mikopo hii kwa kasi kubwa na watamaliza kabla ya muda watakaopangiwa, nami nawaahidi kwamba nitawasimamia,” alisema Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, huku akitoa maombi matatu kwa NMB.
Maombi aliyoyatoa kwa ni pamoja na kusaidia vifaa vya uezekaji wa madarasa yanayovuja ya Skuli ya Tasini (ilipofanyika hafla ya uzinduzi huo), kusaidia maboresho ya miundombinu ya Skuli zilizoathiriwa na upepo mkali na kuezuliwa mapaa kutokana na mvua, pamoja ununuzi wa mshine ya ‘ultra sound’ katika Hospitali ya Kiwani.
Kwa upande wake, Mponzi aliipongeza Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Dk. Mwinyi kwa mchakato endelevu wa Uchumi wa Buluu, huku akibainisha kuwa siri ya ushirikiano mkubwa uliopo baina ya NMB na SMZ ni uzuri, ubora na umuhimu wa maono, mipango na malengo ya Serikali hiyo, yanayowasukuma kuguswa nayo na kupambana kuyasaidia utimilifu wake.
“SMZ ilituonesha ilivyo na mipango ya kuvutia, na kimsingi imefanya makubwa hadi sasa. Nasi tunatumia fursa hiyo kuisapoti na kutokana na mazingira wezeshi iliyoyaweka, imetuwezesha kutanua mtandao wetu wa matawi Zanzibar na Pemba, huku tukijiandaa kufungua tawi jipya Wete, hapa Pemba, lengo ni kufikisha huduma kwa jamii na kuharakisha maendeleo yao.
“Hapa tunakabidhi boti tano zenye nyavu na vifaa vya usalama (maboya, ‘life jacket’ na bima), kupitia ‘NMB MastaBoti’ ambayo imekuja kuwawezesha wavuvi wa kada zote ambao tunajitoa kuboresha mazingira yao ya utendaji kazi. Huu ni mwanzo, kadri watakavyolipa kwa haraka, ndivyo tutavyowafikia wavuvi wengi zaidi,” alisema Mponzi.
Aliwataka Juwaki kutowaangusha wana Kiwani wenzao kwa kulipa marejesho kwa wakati, akitoa wito kwa Wazanzibar kufungua akaunti za benki hiyo ili sio tu kunufaika na huduma mbalimbali ikiwemo mikopo nafuu isiyo na dhamana ya Mshiko Fasta, bali kuchangia pato la jumla la benki hiyo na kuongeza asilimia moja inayotoa kila mwaka kurejesha kwa jamii.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Waziri wa Uchumi wa Buluu, Suleiman Masoud, Waziri wa Maji na Nishati, Shabib Hassan Kaduara, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Khatib Juma Mjaja, Mbunge wa Kiwani, Rashid Abdallah Rashid, pamoja na Mkuu wa Biashara NMB Zanzibar, Naima Shaame na Mkuu wa Idara ya Kilimo NMB, Nsolo Mlozi.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika