January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar: Muungano umeleta amani na utulivu nchini

Na Salma Lusangi, Zanzibar 

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah amesema  Muungano wa Tanzania umeleta mambo mengi ya maendeleo lakini jambo kubwa zaidi ni amani na utulivu iliyonchi nchini.                                                                     

Makamu wa Pili wa Rais, amesema hayo wakati akifungua Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanzania, katika Ukumbi wa Golden Trulip, Kiembesamaki, ambapo amesema wananchi hawana budi kuwashukuru viongozi wawili Marehemu Sheik Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuleta dhana ya  kuziunganisha nchi hizi  mbili yaani Tanganyika na Zanzibar kwa lengo la kuleta maendeleo ikiwemo  amani na utulivu.

 Hemed amesema viongozi hao wameziunganisha nchi kwa mambo kumi na moja kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili.   

Aidha  mwaka jana Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imesaini makubaliano na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano  kumaliza kero katika mambo 11 ya Muungano.  

“Katika maadhimisho hayo, mada zitakazotolewa zitasaidia kuelimisha wananchi ili kuelewa faida zinazopatika katika mambo ya muungano.”  Amesema Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah

Hemedi ameongeza kuwa kuna baadhi ya watu hawazungumzii kwa uhalisia faida zilizopatikana bali wanazungumzia kwa maslahi yao hivyo amewasihi waaalikwa na wananchi wote wanaofuatilia kupitia vyombo vya habari kusikiliza kwa makini mada zote  zitakazowasilishwa .

Naye mtoa mada inayohusu faida za muungano, Wazini wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt Khalid Salum Mohammed, amesema  mambo ya muungano kwa sasa amefikia 22 na yako kikatiba katika jedwali la kwanza.          

Amesema katika mambo hayo maendeleo yamepatika ikiwemo kuimarika kwa ulinzi na usalama, uchumi hali ambayo imesaidia kuwa na sarafu moja ya Tanzania ambapo imesaidia kupunguza gharama kwa Zanzibar. 

Pia amesema  masuala ya ajira kwa katika Taasisi za Muungano, ambapo Wanzanzibar wanapata ajira asilimia 21 kwa taasisi za muungano. Vile vile Dkt Khalid alizungumzia kuimarika kwa utawala bora, miradi ya uviko, na mikopo ya elimu ya juu.        

Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yameandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Raisi kupitia kitengo cha Uratibu shughuli za SMT na SMZ.