Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Othman Masoud Othman, Leo Ijumaa, Oktoba 13, 2023 amewasili huko Wilaya Ndogo Tumbatu Jongowe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwaajili ya kushiriki katika Hafla Kubwa ya Maulid Matukufu ya kila Mwaka ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Othman yupo Tumbatu kwa Ziara Maalum ya Siku Mbili, inayoambatana pia na Ushiriki wa Hafla nyengine ya Maulid, Kesho Jumamosi, huko Tumbatu Kichangani, pia Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Jioni hii, Mheshimiwa Othman amejumuika pamoja na Waumini wa Kiislamu, hapo Viwanja vya Uga Ukuu Tumbatu Jongowe, katika Dhikri na Maulid Mashuhuri ya Kigumi yaliyoandaliwa na Waislamu wa Kijiji hicho.
Hafla hiyo iliyoanza na kisha kuakhirishwa kwa Dua iliyosomwa na Sheikh Khamis Ngwali, ilishuhudia pia Qur-an Tukufu, Zafa, Milango ya Barzanj, na Qaswida kutoka Almadrasat Nurul Munawwarah, na Zawadi za Anasheed zilizoongozwa na Madrasat Jawhar, ya zote kutoka Jongowe, Wilaya Ndogo ya Tumbatu.
Katika Salamu zake, Mheshimiwa Othman ameshukuru Mapokezi ya kipekee ambayo amesema ni vigumu kuyapata kwengineko, ‘vyenginevyo yatakuwa ni mchovyo’.
“Lakini jambo kubwa jengine muhimu tunadumisha utambulisho na utamaduni wetu, kwamba kuna mambo ambayo yanatutambulisha pindipo tukiendeleza Maadhimisho haya na uasili wetu huu”, amesema Mheshimiwa Othman.
Amesema kwamba mtu asiyekuwa na utambulisho inakuwa wepesi kwake kupoteza na kuachana na hata Misingi ya Dini yake.
Amebainisha kuwa kuachana na Uasili pamoja na Miongozo ya Dini, matarajio ni kwa jamii kutumbukia katika khasara., jambo ambalo pia litapekea majuto, kama ambavyo ulimwengu unashuhudia sasa.
Aidha amewahamasisha akinamama kuongeza juhudi katika malezi mema na matunzo ya watoto, akisema, “ukiona pahali pametengenea katika malezi bora ndani familia na jamii kwa ujumla, elewa kwamba kuna juhudi za mwanamke”.
“Naomba hili tuliendeleze; utamaduni huu tusiuache; siku tukiacha uasili huu, tutambue kwamba tutakuwa tumepoteza utambulisho wetu”, amefahamisha Mheshimiwa Othman.
Hivyo amesema ni wajibu kuyaimarisha na kuyaendeleza kwa vitendo Maadhimisho hayo ya Asili, kwani kufanya hivyo ni kutukuza Mwenendo wa Dini ya Kiislamu na Mwongozo aliokuja nao Kiongozi wa Umma huu, Mtume Muhammad (S.A.W.).
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, ameeleza faraja iliyopo kutokana na Hafla hizo muhimu, hasa kwa mnasaba wa upekee unaolenga kudumisha na kuendeleza Mila na Silka za Asili, kutoka kwa Wazanzibari.
Masheikh, Waumini, Vijana wa Madrasa, Walimu na Wanafunzi, Makundi ya Wananchi, Kike kwa Kiume, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Ayoub Mahmoud Mohammed, wamejumuika kumpokea Mheshimiwa Othman Kijijini hapo.
Viongozi wengine waliojumuika hapo, wakiwemo kutoka Vyama vya Siasa, ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Bw. Sadifa Juma Khamis; Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Mambo ya Siasa, Bw. Haji Omar Kheri; na Kiongozi wa Twarika ya Nakshaband, Sheikh Jabir Haidar Aljabry.
Kwa ujumla Hafla zote hizo za tangu asili na zama, huwajumuisha Wananchi na Waumini kutoka Maeneo mbalimbali ya Unguja, Pemba, Tanzania Bara na hata Nje ya Nchi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi