Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Leo Jumamosi Agosti 17, 2024,ameshiriki akiwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Programu ya Kuirithisha Zanzibar ya Kijani (Zanzibar Green Legacy Program), huko Viwanja vya Maonyesho ya Biashara, Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Hafla hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kwa Mashirikiano ya Wadau mbali mbali wa Mazingira, ndani na nje ya Nchi.
Uzinduzi wa Programu hiyo yenye Dhamira ya Kuyahuisha Mazingira na Uoto wa Asili wa Visiwa vya Unguja na Pemba, umebeba Kaulimbiu isemayo, “Zanzibar ya Kijani Inawezekana; Shiriki Kupanda na Kuitunza Miti”.
Akitoa salamu zake mbele ya Hafla hiyo, Mheshimiwa Othman amesema Nchi ipo hatarini ikikabiliwa na Athari kubwa za Mazingira zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi, kutokana na jamii kutoelewa umuhimu wa misitu, na kutowajibika ipasavyo katika kuendeleza urithi na utamaduni wa asili, wa kupanda na kuitunza miti.
Amesema, Kizazi cha Sasa kimeelekeza nadhari zao katika matumizi na kuihujumu misitu, na siyo kuitunza na kuiendeleza, hali ambayo ni tofauti na juhudi za Wazee pamoja na Kizazi Kilichopita, kilichowekeza katika kujenga Mazingira mazuri na Urithi wa Asili.
Mheshimiwa Othman amesema Programu hiyo itainufaisha Jamii ya Zanzibar kwa ujumla, kwa kupunguza uwezekano wa kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, na hasara nyengine za kimazingira.
Akisisitiza ufanikishaji wa Lengo Kuu la Programu hiyo Mheshimiwa Othman amesema, “shabaha ya kila mwaka ni kupanda na kuitunza Miti Milioni Tatu (3,000,000) katika maeneo yote ya Unguja na Pemba, ikiwa ni pamoja na Miti ya Mikoko ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu ya Uchumi wa Buluu; na kwa kuzingatia kwamba tumekuwa na tabia ya kupanda pekee, na hatuitunzi miti tunayoipanda; hivyo Mpango huu unaweka msisitizo wa mambo yote mawili, kuipanda na kuitunza, ili kuhakikisha kuwa miti itakayopandwa inakuwa na kunawiri vizuri”.
Kupitia Hafla hiyo Mheshimiwa Othman amewaomba Wananchi, Taasisi za Serikali na Zisizo za Kiserikali, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Wafanyabiashara, Wawekezaji, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Wanadiplomasia, Ofisi za Kibalozi, Wanamichezo, Wasanii, Wanahabari, Vyama vya Siasa, Taasisi za Elimu na Wanataaluma, Viongozi wa Kidini, na kila Mtu, kuangalia namna bora ya kushiriki katika Programu hiyo ili kuirejesha Zanzibar kwenye Asili na Urithi wake wa Kijani.
Hivyo amesema ni jukumu la kila mmoja kuwajibika ipasavyo katika kujenga utamaduni na tabia endelevu ya kupanda, kutunza, kuhifadhi na kuendeleza miti ya matunda, misitu na mikoko, mijini na vijijini, na kuimarisha uoto wa asili kwa ujumla, ili kurejesha haiba na urithi wa mazingira ya asili, kwaajili ya maendeleo endelevu na kwa maslahi ya Uchumi wa Nchi.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Harusi Said Suleiman, amesema Mradi huo ni faraja kubwa kwa Nchi, kwani ni Urithi wa Matumaini kwa Vizazi vya Sasa na Baadae.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, ameshukuru na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali, hasa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa kuleta Mpango huo ambao manufaa yake ni kwa Sekta zote za Maendeleo, pamoja na Wananchi kwa ujumla.
Akitoa Maelezo Mafupi ya Kitaalamu juu ya Mpango huo, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ndugu Ilyasa Pakacha Haji, amesema lengo ni kuwepo Juhudi Jumuishi, zinazohusisha Sekta mbali mbali za Serikali na Binafsi, ili kuhakikisha Utekelezaji wa
Sera za Taifa zinazohusu Mazingira, zinafanikiwa.
Viongozi mbali mbali wa Serikali, Mawaziri, Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Mawaziri na Mawaziri Wastaafu, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Maafisa Wadhamini, Wadau wa Mazingira, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Asasi za Kiraia, Wawakilishi wa Makampuni na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, pamoja na Wananchi, wamehudhuria katika hafla hiyo, wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa; Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said; na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendeshaji na Usimamizi wa Mazingira Zanzibar, Bw. Sheha Mjaja Juma.
Hafla hiyo imehusisha harakati mbali mbali, ikianza na Dua iliyosomwa na Sheikh Mziwanda Ngwali kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar; Maelezo Mafupi juu ya Mtazamo wa Dini katika Kuyatunza Mazingira, yaliyotolewa na Sheikh Abdul Simba; Zoezi la Upandaji wa Miti na uwasilishaji wa Documentari inayoonesha maudhui ya mpango huo hapa visiwani.
Awali, Mheshimiwa Othman amezindua tovuti maalum ya Programu hiyo itakayotoa fursa kwa watu binafsi, taasisi, mashirika na jamii kujisajili kwaajili ya ushiriki na utekelezaji wake.
Katika Hafla hiyo Mheshimiwa Othman ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa