Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Leo Agosti 12, 2024, huko Ofisini kwake Migombani,Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, amekutana na kufanya Mazungumzo na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania.
Ujumbe huo ambao umeongozwa na Naibu Balozi wa Marekani Nchini,Andrew Lentz, umefika kuonana na Othman kwa Lengo la Kujitambulisha na Kubadilishana Mawazo juu ya Mambo mbali mbali, yakiwemo Siasa, Uchumi, Maendeleo na Mustakbali wa Nchi, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Katika Mazungumzo hayo,Othman amesema ni jambo la muhimu na lisiloepukika kurudisha imani za Wananchi wa Zanzibar, ili kujenga mustakbali mwema wa Amani, Uchumi na Maendeleo Nchini na katika Tanzania yote.
Amesema tangu nchi iliporudi tena kufuata Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Zanzibar haijawahipo kuwa na Uchaguzi ulioacha furaha kwa pande zote na badala yake huacha vilio, machungu na makovu ambayo kwa kiasi kikubwa yanawapata Wananchi Wafuasi wa Upinzani, jambo ambalo halileti afya njema kwa mustakbal wa amani na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Ili kuifanya Zanzibar na Wazanzibar na kurudisha imani yao kwa Serikali na Mamlaka zinazotawala na pia kuondoa hofu na mifumo dhalimu ya Uchaguzi, hakuna namna zaidi ya kuwa na dhamira njema ya kisiasa na kutekeleza demokrasia kwa vitendo” amefahamisha Othman.
Akitaja maeneo ambayo yanahitaji marekebisho ya haraka kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Mheshimiwa Othman amebainisha mambo kadhaa yakiwemo Haki ya Kisheria ya Kuwapatia Wananchi Vitambulisho vya Mzazibari (Zan ID); Uandikishaji wa Haki ndani ya Daftari la Kudumu la Wapigakura (PVR); Kuondoa Wapigakura Mamluki wa Kughushi (ghost voters); Kuepusha wizi wa Kura kupitia Uchaguzi wa Siku Mbili Zanzibar; Kuwepo na Tume Huru ya Kusimamia Demokrasia, Uchaguzi wa Haki na Kuheshimu Maamuzi ya Wananchi kupitia Sanduku la Kura; na pia Kuachana na Matumizi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama katika Kupora Uchaguzi kwa ujumla.
Aidha amesema katika kuimarisha Uchumi wa Nchi, Zanzibar inahitaji uwajibikaji na uwazi, ili kufungua pia fursa za Uwekezaji kutoka Nje, huku akisisitiza kwa kusema, “siku zote muwekezaji huwekeza katika amani”.
Mheshimiwa Othman, ameiomba Serikali ya Marekani kuendelea kutoa ushirikiano ili kuisaidia Serikali ya Zanzibar katika kufanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, utakaopelekea kujitegemea na kuongeza kasi ya maendeleo, sambamba na kusaidia utekelezaji wa Sera ya Uchumu wa Buluu.
Mhehimiwa Othman amebainisha pia uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi pindipo kukiwepi na mikakati thabiti ya kuwawezesha vijana na kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira; na wala siyo zile ghilba za kuitumia sehemu hiyo muhimu ya jamii katika kuhujumu Uchaguzi kwa maslahi ya wanasiasa wachache wanaoendekeza zaidi matumbo yao.
Hivyo amesema iwapo vijana watajengewa uwezo katika nyanja mbali mbali mathalan uvuvi, kilimo na ufugaji, wataweza kujiajiri, kuzalisha mali, na hatimaye kujiendeleza vyema katika kuleta maendeleo na kusaidia katika pato la Taifa.
Naye, Balozi Andrew ameahidi kuendeleza mashirikiano kati ya Nchi yake na Zanzibar, pamoja na Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kupata ithibati juu ya imani na amani yao kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Amesema akiwepo Zanzibar yeye na Ujumbe wake, pamoja na mambo mengine wamekuwa na mazungumzo na vijana kadhaa, ambao baadhi yao wameonyesha hofu juu ya viashiria vya kile ambacho kinaweza kujiri katika Uchaguzi Mkuu wa hapo Mwakani.
Watendaji na Maafisa mbali mbali wa Serikali, pamoja na wale kutoka Ubalozi wa Marekani wamehudhuria katika Kikao hicho, wakiongozwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Ilyasa Pakacha Haji.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito