December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makalla amtaka Mkandarasi kuongeza kasi ujenzi Hospitali ya Mbagala Rangi tatu

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ameridhishwa na ujenzi wa hospitali ya ghorofa sita ya Mbagala Rangi tatu ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu kiasi cha Sh.Bil 10.

Amemuagiza Mkandarasi anayejenga hospitali hiyo kutoka Group Six Internation Limited kuongeza kasi ya ujenzi ili ikamilika kwa wakati.

Akitembelea na kukagua mradi wa jengo hilo la Hospitali leo Agosti 29, 2024 Jijini Dar es Salaam, akiwa kwenye ziara yake ya kichama, CPA Makalla amesema ameridhishwa na mwenendo wa hospitali hiyo na kudai kuwa, kukamilika kwake kutaenda kupunguza hadha ya wakazi wa Mbagala pindi wanapotaka kupata huduma za kiafya.

Amesema ni vyema wananchi wa Wilaya ya Temeke, hususani wakazi wa Mbagala wakatambua na kunufaika na jitihada zinazofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa kuleta mradi huo ambao hadi sasa umefikia asilimia 60 na kutarajiwa kukamilika Juni 2025.

“Napenda kuendelea kumshukuru Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Kufuatia kukamilika kwa mradi huu kutaenda kupunguza hadha kwa wananchi pindi watakapotaka kupata huduma za kiafya na watapata hapa katika Hospitali hii ambayo itakuwa ya ngazi ya Wilaya na itaenda kuhudumia Kata mbili tulizotajiwa na maeneo mengine jirani”, amesema CPA Makalla.

Awali akitoa taarifa ya Mradi huo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Jonas Lulandala amesema, Wilaya ya Temeke ina Vituo vya Afya 179, huku akisema kati ya hivyo Vituo vya umma 30, binafsi 133, Dini 17 na Serikali mbili.

Pamoja na mradi huo alitembelea mradi  mwingine ambapo alikagua ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Mangaya, iliyopo katika Jimbo la Mbagala unaoenda kugharimu zaidi ya Sh. Mil 800.

Shule ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 800, itakuwa na vyumba vya madarasa 16, matundu ya vyoo 48 na ofisi nane za walimu.