October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makalla amtaka Mganga Mkuu Dar es Salaam kufuatilia malalamiko Hospitali ya Nguvu Kazi

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online Dar

KATIBU wa NEC, Siasa, itikadi, Uenezi na mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, amemtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Zaituni Hamza, kufuatilia mwendo unaolalamikiwa na wananchi kuwa mbovu katika Hospitali ya Nguvu kazi, iliyopo Chanika Jijini Dar es Salaam.

Kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi walio hudhuria katika mkutano wa hadhara wa Katibu Mwenezi, uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Chanika, wameilalamikia Hospitali hiyo kuwatiza pesa wajawazito pindi wanapofika kupatiwa huduma, kuwatoza pesa pindi wanapoenda kujifungua na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutozwa pesa pindi wanapopatiwa huduma ya matibabu.

Baadhi ya wananchi hao, ambao hawakutana Majina yao kuchapishwa kwenye vyombo vya habari, walisema ” Tunashukuru sana Mwenezi leo umekuja na wewe ukiwa kama Mlezi wa CCM tunatumia itatudaidia kutatua kero zetu.

Zipo kero nyingi sana, ikiwa pamoja na kuwepo kwa watendaji wasiyo kuwa na maadili katika Hospitali yetu ya Nguvu Kazi, pale tunapatiwa huduma mbaya labda mpaka utoe chochote kitu, wajawazito tunatozwa pesa pindi tunapoenda kupata huduma ya kliniki, pia hata ukienda kujifungua ukitaka kuhudumiwa haraka na vizuri ni lazima utoe pesa, lakini pia watoto wetu wenye umri chini ya miaka mitano hawatibiei bure hadi utoe pesa”, alisema mmoja wa wananchi hao.

Pia, wameilalamikia hospitali hiyo kuwa na mfumo mbovu wa uchomaji taka, hali inayowasababishia wakazi wa maeneo ya jirani kuathirika kiafya kutokana na moshi unatokana na taka hizo.

Wakati akisikiliza na kutatua kero hizo, Makalla amemtaka Mganga Mkuu katika Halmashauri hiyo kufuatilia jambo hilo kwa haraka, huku akieleza kuwa Chama cha CCM kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa majibu na kuelezea kuwa huo ni wajibu wa Chama hicho.

“Niendelee kusema kuwa, Chama cha CCM kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kero za wananchi zinasikulizwa na kutatuliwa kwa wakati na hiyo ndiyo dhima ya CCM kutatua kero za wananchi na si kuzikimbia, hivyo nitoe wito kwa watendaji wote Serikalini kutimiza wajibu wenu katika kutoa huduma nzuri kwa wananchi na kufanya hivyo ndiyo siraha ya chama, hivyo kwa hili la Hospitali naomba DMO kesho ufike kwenye hiyo hospitali na kufuatilia malalamiko yote na kufanyia kazi”, amesema Makalla.

Aidha, Makalla amewahakikishia Wakazi wa Jimbo la Ukonga kuwa, katika uchaguzi wa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, Chama hicho kitawasimamisha wagombea wanaokubalika na wenye kiu ya kutatua Changamoto za Wananchi na si vinginevyo.