June 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:Wanufaikaji Mikopo ya Elimu ya Juu kuongezeka

▪️Asema Rais Dkt. Samia amedhamiria kuendelea mazingira ya Elimu ya juu.

▪️Asisitiza Samia Scholarship pia kuwafikia wengi zaidi.

▪️Rais wa TAHLISO asisitiza Oktoba Wasomi wako tayari kuilinda amani kuelekea uchaguzi mkuu.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika mwaka 2025/2026 Serikali imepanga kutoa mikopo kwa wanafunzi 252,773 wakiwemo 88,320 wa mwaka wa kwanza ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.

Amesema hayo leo Jumamosi (Juni 14, 2025) wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu, yanayofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma

“Huu ni muendelezo wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha elimu ya juu na mazingira ya wanafunzi kwa ujumla, Mwaka 2024/2025, mikopo ya shilingi bilioni 787.4 imetolewa kwa wanafunzi 248,331 ikilinganishwa na bilioni 570 kwa wanafunzi 177,925 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 40”.

Kwa upande wa Ufadhili wa Samia (Samia Scholaship) Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 wanafunzi 2,630 watapatiwa Ufadhili wa kupitia progamu hiyo ambayo mpaka sasa jumla ya wanafunzi 1,976 wananufaika na ufadhili huo . “Programu hii ni kwa ajili ya wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha Sita katika masomo ya Sayansi”.

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuleta unafuu katika urejeshaji wa mikopo, Serikali imeondoa adhabu na tozo ya kulinda thamani katika urejeshaji wa mikopo kwa lengo la kuongeza unafuu kwa wahitimu. “Hatua hii imeongeza marejesho ya mikopo. Vilevile, imetengenezwa Mfumo wa Marejesho unaotumika na taasisi 3,565, na mfumo wa utambuzi unaotumika na wanufaika takriban 3,000 kwa mwezi.”

Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa utaratibu wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika mwaka 2023/2024 mpango huo ulianza kwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 7.29 na mwaka 2024/2025 ziliongezwa hadi kufikia shilingi bilioni 19.95 sawa na ongezeko la asilimia 177.6.

“Mpango huu unahusisha fani za kipaumbele ambapo jumla ya wanafunzi 13,214 wamenufaika hadi sasa”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanavyuo wote nchini kutokubali kutumika na baadhi ya wanasiasa wenye nia ovu ya kuwavuruga na kilifanya Taifa liishi bila amani “Tanzania ni yetu, endeleeni kuhakikisha kuwa Taifa hili linabaki salama pamoja na uchaguzi tulionao mbele yetu”

Kadhalika ametoa wito kwa viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) kuhakikisha wanahimizana kuwa mfano mzuri kwa jamii. “Tambueni kuwa Taifa zima linawaangalia ninyi kama kioo cha jamii, jiepusheni na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya Kitanzania ikiwemo ushoga, usagaji, na matumizi ya madawa ya kulevya”

Naye, Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Qs Omar Kipanga amesema Wizara hiyo inaendelea na mpango wa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 yenye kulenga kutoa elimu inayozingatia ujuzi kulingana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

“Katika kufanikisha utekelezaji wake, tumefanikiwa kuhuisha mitaala na kuandaa miongozi mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inazingatia viwango vya kitaifa, kimataifa na kuwajengea wahitimu ujuzi unaohitajika katika karne ya 21.”

Kwa Upande wake Rais wa Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Geofrey Kiliba amesema kuwa taasisi hiyo inaishukuru Serikali kwa maboresho makubwa katika sekta ya elimu ya juu, Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi kuanzia miundombinu, kuongezeka kwa bajeti ya mikopo, kuimarisha kwa mitaala na usimamizi bora wa vyuo na taasisi za elimu ya juu

“Sisi TAHLISO tupo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika nyanja zote ikiwemo kisera na kielimu ili kuchochea maendeleo makubwa zaidi kwa Taifa letu”