WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 8.04 ambazo ni sawa na sh. trilioni 18.58 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni moja mwaka 2020/2021.
“Mafanikio hayo yanatokana na ziara mbalimbali za viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alizozifanya nje kwa lengo la kuifungua nchi. Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira takriban 62,301,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 6, 2022) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuvutia na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini. “Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji, kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazosimamia uwekezaji pamoja na kutenga hekta milioni 1.6 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 ili iendane na mazingira ya sasa ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kujumuisha vipaumbele vilivyoainishwa katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuondoa muingiliano wa majukumu kwa taasisi za udhibiti, kuondoa tozo sumbufu na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi. “Aidha, itaimarisha majadiliano na utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta binafsi.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 922,692 mwaka 2021.
Waziri Mkuu amesema utalii wa ndani pia umeendelea kuimarika ambapo idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi iliongezeka kutoka 562,549 mwaka 2020 hadi 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2.
Amesema Serikali imeongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa, kuboresha ulinzi na usalama wa rasilimali za maliasili na malikale na kushirikisha jamii katika kutekeleza mipango ya uhifadhi wa ikolojia.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zimekuwa chachu ya kuongezeka kwa mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 1.25 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba