November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:Mikataba ya uendeshaji wa Bandari kuzingatia maslahi ya nchi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha kuwa mikataba ya utekelezaji wa makubaliano ya uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World itazingatia maslahi ya nchi na kuleta manufaa kwa Taifa.

Akizungumza wakati akiahirisha Mkutano wa Bunge jijini Dodoma.Waziri Mkuu huyo amesema, makubaliano yaliyoingiwa yanalenga kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai 

Amesema kwa kuwa bandari ya Dar es salaam ndiyo kitovu cha huduma za bandari nchini Serikali iliamua kutafuta Kampuni yenye uwezo na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa bandari duniani kwa teknolojia za kisasa ili kuiwezesha bandari hiyo kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza mapato ya nchi na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi. 

Aidha amesema Serikali za Tanzania na Dubai zimeingia makubaliano kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na wa kijamii katika uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kupitia Kampuni ya DP World, ambayo imeonesha kuwa na utaalamu, uwezo na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa bandari 190 katika nchi 68 barani Afrika, Asia, Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Kusini.

Juni10, 2023 Bunge lilijadili na kupitisha azimio la mapendekezo ya kuridhia makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini.

 Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa,Mamlaka ya Bandari  Tanzania imekasimiwa haki ya kuwa mmiliki wa maeneo yote ya bandari nchini na haina uwezo wa kutoa umiliki huo kwa kampuni nyingine.

“Kuhusu umiliki wa bandari , nilihakikishie bunge lako na wananchi kwa ujumla kwamba, kupitia Sheria ya Bandari ya Mwaka, 2004,kwamba Mamlaka ya Bnadari imekasimiwa haki ya kuwa mmiliki wa maeneo yote ya bandari nchini na haina uwezo wa kutoa umiliki huo kwa kampuni nyingine.”amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa

“Haki iliyopewa kwa mujibu wa sheria hiyo ni kuingia mikataba ya ushirikiano wa kupangisha na kuruhusu sekta binafsi kuendesha sehemu ya maeneo hayo.” 

“Sote tunafahamu kuwa, bandari ya Dar es salaam ndiyo kitovu cha huduma za bandari nchini. Ili kuiwezesha bandari hiyo kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza mapato ya nchi, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi, Serikali iliamua kutafuta Kampuni yenye uwezo na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa bandari duniani kwa teknolojia za kisasa,

“Makubaliano yaliyoingiwa yanalenga kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali yetu na Serikali ya Dubai,na maeneo ya uwekezaji yatakayopendekezwa yataingiwa mkataba kwa kila eneo hivyo, masuala ya mfumo wa uwekezaji, mgawanyo wa mapato, muda wauwekezaji na ukomo yatajadiliwa kwa kina.”amesea Waziri Mkuu Majaliwa

Waziri Mkuu amesema wakati wote wa utekelezaji wa makubaliano hayo na mikataba itakayoingiwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza majukumu yao katika eneo la mradi kama vilivyofanya katika kipindi cha miaka yote 22 ya mkataba na mwekezaji wa awali (TICTS) aliyemaliza mkataba wake.

 “Kuhusu mapato, ninapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kusimamia masuala ya mapato ya Serikali kutoka kwa mwekezaji kwa mujibu wa sheria na mkataba.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kupokea mapendekezo, maoni na ushauri kutoka kwa waheshimiwa wabunge, wananchi na wadau mbalimbali. Ametumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iendelee kuratibu utoaji wa elimu na ufafanuzi wa hoja za wananchi huku akitoa rai kwa watanzania kutoruhusu mgawanyiko wa aina yoyote ile wanapotoa maoni yao kuhusu uwekezaji wa bandari.

“Lakini pia tuepuke kujadili itikadi za kisiasa, udini, ukabila, ukanda au vyovyote vile, muhimu tuenzi tunu yetu ya amani na mshikamano wa Taifa letu iliyojengwa na waasisi wetu.”