January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Polisi hakikisheni hakuna wizi wa vifaa ujenzi wa reli Mwanza-Isaka

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Misungwi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Misungwi kuhakikisha hakuna vifaa vitakavyoibiwa katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kipande cha tano kutoka Mwanza-Isaka ambao umefikia asilimia 14.

Waziri Mkuu huyo Majaliwa,ametoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi mradi wa huo katika kituo cha reli cha Fela wilayani Misungwi,ambapo yupo mkoani Mwanza kwa ziara ya kawaida ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na serikali.Majaliwa ameeleza kuwa, kuna tatizo ambalo wameanza kuliona hapo katika mradi huo la wananchi kudokoa vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo ikiwemo nondo,saruji na mafuta ya magari.

Hivyo Jeshi la Polisi linatakiwa kuhakikisha Mkandarasi wa mradi huo awakwamishwi kukamilisha mradi kwa sababu ya wizi wa vifaa.

“Niwaambie hilo halikubaliki natoa wito kwa Jeshi la Polisi Mkoa na Wilaya hakikisheni kampuni hii inayotekeleza mradi huu haipotezi mali zao wanapotujengea reli yetu Watanzania, na yoyote atakaye ingia kwenye wimbi la wizi wa vifaa vya ujenzi hatua kali za kisheria zichukuliwe,sisi hatutoridhika kuona mradi una kwama eti kwa sababu miongoni mwetu kuna ambao hawapendi kuona mradi ukiendelea,”ameeleza Majaliwa.

“Serikali na Rais wetu wameridhia kutoa pesa nyingi leo tuje tutengeneze hasara haikubaliki, wanaMisungwi kila mmoja awe mlinzi wa ujenzi wa reli hii kusiwe na mtu anaiba saruji humu,mtu akikuuzia saruji muulize ameipata wapi saruji inapatikana dukani siyo mkononi mwa mtu,”.

Pia amewataka mafundi wote ambao wameshiriki katika mradi wa ujenzi huo pindi utakapo kamilika wawe wamekuwa mahili katika ufundi kulingana na kitengo alichokuwa anafanya kazi huku akitolea mfano kama ni fundi wa kuvunja nondo basi awe mahili katika kipengele hicho.

“Wito wangu kwenu kila mmoja kwa nafasi yake mradi utakapo kamilika muwe mafundi mahili,ili tukitaka kujenga reli nyingine tusiagize mafundi kutoka nje nyie ndio muwe mafundi wa reli hiyo nyingine, tumefanikiwa sana kwa kipande cha Dar-es-Salaam,Pwani na Morogoro wamezalisha mafundi wengi sana na ndio hao wameingia kwenye kipande cha nne, hakikisheni na nyie mnaenda kipande cha sita na saba,”amesisitiza Majaliwa.

Aidha amemuhimiza Mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kufanya kazi kwa saa 24 na kuongeza nguvu kazi ili mradi huo ambao unapaswa kukamilika Mei,24,2024 ukamilike mapema zaidi.

Sanjari na agizo hilo pia Waziri Mkuu amewataka wananchi wa Misungwi kutumia fursa ya eneo la kituo cha reli cha Fela ambacho kitakuwa bandari ya nchi kavu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kufanya uwekezaji kwa kujenga hoteli na nyumba za kulala wageni ili kujiinua kiuchumi.

Vilevile Waziri Mkuu ameeleza katika mradi huo katika maeneo ya Jiji itajengwa reli ya juu huku chini zikiwa barabara ili kuepuka kubomolea wananchi nyumba.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameeleza kuwa reli yote imejengwa kwa kiwango cha kimataifa na ikikamilika kutoka Dar-es-Salaam hadi Mwanza itakuwa na urefu wa kilomita 1219 ambapo itatumia saa 8.Mhandisi Kasekenya ameeleza kuwa kwa kipande hicho cha tano cha reli kutoka Mwanza-Isaka,kitatumia kiasi cha tirioni 3.12 mpaka kukamilika kwake huku utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 14.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC),Amina Lumuli ameeleza kuwa katika kipande hicho wanategemea watalaza reli takribani 500,000, hadi kukamilisha ujenzi mradi huo ambacho kitakuwa na vituo(station) 10 ikiwemo ya Fela ambacho kitakuwa bandari ya nchi kavu.

“Jumla kwa vipande vyote vitano mradi utatumia kiasi cha tirioni 16.17, kipande hiki kitatumia tirioni 3.12 na serikali kwa ujumla imeisha lipa kwa kazi zote ambazo zimeisha fanyika kwenye mradi mzima kiasi cha zaidi ya tirioni 6 na utapunguza muda wa safari kutoka Dar-es-Salaam hadi Mwanza kutoka masaa 20 hadi 8 pia utapunguza gharama za usafiriji wa mizigo kwa asilimia 30-40,”ameeleza Amina.

Muonekano wa reli ya kisasa kipande cha tano Mwanza-Isaka,pindi mradi wa ujenzi huo utakapo kamilika.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,akisikiliza maelekezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha tano Mwanza-Isaka, wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi mradi wa huo katika kituo cha reli cha Fela wilayani Misungwi,ambapo yupo mkoani Mwanza kwa ziara ya kawaida ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na serikali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Misungwi(hawapo pichani) mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha tano Mwanza-Isaka, wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi mradi wa huo katika kituo cha reli cha Fela wilayani Misungwi,ambapo yupo mkoani Mwanza kwa ziara ya kawaida ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na serikali.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Misungwi waliojitokeza wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,alipotembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha tano Mwanza-Isaka, wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi mradi wa huo katika kituo cha reli cha Fela wilayani Misungwi,ambapo yupo mkoani Mwanza kwa ziara ya kawaida ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na serikali.