Magesa, Judith Ferdinand, Times Majira Online, Ukerewe
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahaidi wananchi wa Kisiwa cha Irugwa Wilayani Ukerewe kituo cha afya, boti, kivuko na kuboresha huduma za jamii, shule za msingi na sekondari.
Hatua hiyo itawafanya wakazi hao wapate huduma karibu na kuwapunguzia umbali wa kusafiri na gharama za kufuata matibabu jijini Mwanza huku boti, kivuko na kuboresha huduma za jamii kwenye sekta ya maji na miundombinu ya shule katani humo.
Ahadi hiyo aliitoa kwenye mkutano wa kampeni wakumuombea kura mgombea Urais wa CCM. Dk. John Magufuli, uliofanyika katika Kijiji cha Nabweko kisiwani Irugwa,wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.
Akihutubia umati wa wananchi wa kisiwa hicho, Majaliwa amesema hawana budi kuichagua serikali ya CCM iendelee kuleta maendeleo, kutatua changamoto zao na kuwahudumia kwa dhati.
Amesema, kisiwa cha Irugwa na wilaya ya Ukerewe kina changamoto ya huduma za afya, hivyo baada ya uchaguzi na Rais, wabunge na madiwani kuapishwa kazi ya kwanza ya Mbunge wa Ukerewe ni kuhakikisha kituo cha kwanza cha afya kinajengwa Irungwa ili kuwasogezea huduma na kuwaondolea wananchi adha ya kuzifuata huduma Mwanza.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu amesema ukubwa wa Kata ya Irugwa inahitajika kituo cha afya ili wagonjwa wenye matatizo ya kiafya wapate huduma karibu, nje ya hapo ni gharama na watu kupoteza maisha.
“Nataka niwambie, tumejenga zahanati 1,498 vijijini na vituo vya afya 498 nchi nzima hapa Ukerewe vitatu (Muriti, Kagunguli na Bwisya kwa zaidi ya bilioni 1, kitawapunguzia umbali na gharama za kusafiri na kutumia mitumbwi kufuata huduma, baada ya kuapishwa Mkundi aje kuchukua fedha za vituo vya Ukerewe, cha kwanza kujengwa ni Irugwa,”amesema Majaliwa.
Aidha alidai ujio wake Irugwa mbali na kampeni umelenga kuwajengea kituo cha afya kitakachokuwa karibu na Hospitali ya Bwisya iliyopandishwa hadhi kuwa ya wilaya na itatoa huduma ili kuokoa maisha na kuwapunguzia gharama za kwenda Mwanza na Nansio na yote yako kwenye ilani ya CCM.
Amesema, wote ni mashahidi kazi za maendeleo zilizofanywa na serikali kwa miaka mitano zinaakisi maisha ya watanzania wote na ndiyo maana anamwombea kura Rais Dk. Magufuli, amejipanga kuwatumikia kwa kipindi cha miaka mitano mingine ili malengo yaweze kufikiwa.
“Nchi hii inahataji kupata kiongozi mwenye dhamira ya wazi ya kutunza amani, hayo maendeleo mnayoyaona ni matokeo ya uadilifu wa ukusanyaji kodi na kuisimamia ili itumike kupunguza matatizo ya wananchi, kazi iliyofanywa kwa uadilifu na Dk. Magufuli,”amesema Majaliwa.
Hata hivyo amesema, maji pamoja na wingi wake bado hayatoshi kuwafikia wananchi hadi ndani, mkakati uliopo ni kuwawezesha wapate maji hayo kupitia kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ambapo serikali imeshachimba na itachimba visima vijijini.
Majaliwa amesema, serikali katika miaka mitano iliyopita imetoa bilioni 1.3 za ujenzi wa visima na kuwanufaisha watu wa Kazilankanda, Nansole, Chibulungo, Ihebo, Muriti na Irugwa yenyewe, pia ilitoa bilioni 13 za kutekeleza miradi ya maji kwenye vijiji vya Ukerewe.
Sekta ya usafiri wa majini amesema, licha ya upotoshwaji unaofanywa na wapinga maendeleo serikali itaendelea kuimarisha maeneo ya visiwa kwa kununua meli, boti na kujenga vivuko ambapo itanunua boti itakayohudumia watu wa Irugwa na Bwisya,Ukara, Bukondo-Bwiro na Lugezi Kisorya.
Pia Julai mwaka huu serikali imetoa bilioni 2.4 kuiwezesha TARURA kuboresha barabara za Ukerewe zilizoharibiwa na mvua zipitike muda wote ingawa mbunge aliomba daraja kati ya Lugezi-Kisorya.
“Changamoto ni nyingi lakini tumezipunguza, tumezieleza kazi tulizofanya mmeziona na kuzisikia ndio sababu tunaomwombea ridhaa tena Dk. Magufuli arudi madarakani, anatambua mchango wa wanyonge na changomoto zao hivyo mpeni mitano mingine ,”amesema Majaliwa.
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba