November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa amfagilia Kasekenya

Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Songwe

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amempongeza Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya kwa kusimamia fedha za ujenzi wa mradi wa maji Itumba – Isongole na kupelekea kupata maendeleo zaidi katika mradi huo.

Pongezi hizo amezitoa leo Mkoani Songwe akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo wa maji Itumba-Isongole akiwa katika ziara yake mkoani Songwe.

“Mlipata mkandarasi wa kwanza akajenge tenki kwa 24% lakini mkajifunza kuwa atawashelewesha, ingawa mlimlipa Bilioni 1.4, Mkuu wa Mkoa akachukua hatua ya kusitisha mkataba ili kumpata mkandarasi mwingine. Bado mkabaki na fedha na mkajenga tena matenki mengine mawili likiwemo na hili la hapa Itumba-Isongole, na bado naambiwa una fedha. Kitendo hicho Cha kusimamia fedha kimetufanya kupata maendeleo zaidi” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa

“Tungepata watumishi ambao Si waaminifu wangejenga mradi huohuo ambao umechorwa kwenye michoro kwa Bilioni 4 hizo hizo, lakini hawa Wana Bilioni 4 kwenye mradi huohuo wamejenga matenki mengine mawili, hivyo nakupongeza wewe Naibu Waziri wa Ujenzi na watumishi wenzako wa RUWASA bila kumsahau meneja wa Wilaya ambaye amekuwa akisimamia mradi huu Kila siku”

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwa RUWASA huo siyo mradi wa kwanza kuona namna wanavyotumia fedha kwa umakini na kusimamia ubora wa miradi yenyewe .

“Leo tumepata chanzo cha kwanza kilichokua kinatoa Lita kidogo, kupitia fedha ileile Bilioni 4 mmepata vyanzo viwili na vinatoa maji zaidi Lita Milioni 5, mahitaji zaidi ya Milioni 3, na tuna ziada ya Milioni 1.8 hivyo Eng. Kasekenye kilio chako Cha maji kimekwisha” Amesema Waziri Majaliwa