Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Mbeya
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya NMB kwa kutenga fedha zaidi ya sh. bilioni 40 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kwenye Mpango wa Kuwaandaa Vijana na Wanawake kwa Kesho iliyo Bora (BBT).
Mpango huo ni kupitia kilimo, uvuvi na ufugaji, pamoja na kushuka kwa riba ya mikopo ya sekta hizo za kimkakati hadi kufikia asilimia tisa.
Majaliwa ametoa pongezi hizo alipotembelea Banda la NMB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya, ambapo ameelezwa kuwa katika kipindi cha miaka miwili, benki hiyo imetenga sh. bilioni 40, zikiwemo sh. bilioni 20 za mikopo ya kuunga juhudi za BBT na sh. bilioni 20 zingine ni kwa ajili ya mikopo ya ujenzi wa maghala ya kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno.
Hata hivyo Majaliwa alimuuliza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye alikuwa ameongozana nae kwenye maonesho hayo,ili kujiridhisha kama ni kweli Benki ya NMB imepunguza riba kwenye mikopo ya kilimo hadi kufikia asilimia tisa.
“Mheshimiwa Waziri wa Kilimo (Hussein Bashe), ni kweli kwamba riba ya mikopo ya kilimo, uvuvi na ufugaji
imeshuka kiuhalisia na kufikia asilimia tisa! Hongereni sana kwa kushusha riba kutoka double digit (yaani tarakimu mbili) hadi kufikia single digit (tarakimu moja). Ni matumaini yangu itashuka zaidi hadi asilimia nane au saba (7)” ameuliza na kupongeza Majaliwa.
Awali, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Straton Chilongola alimueleza Majaliwa kuwa kwa miaka miwili, Benki ya NMB imetenga sh. bilioni 40 kwa ajili ya kuunga mkono BBT ikienda sambamba na kupunguza riba hadi asilimia tisa.
Chilongola, pia ameipongeza Serikali kwa kuipa kipaumbele na kuiwekea mazingira wezeshi Sekta ya kilimo, Uvuvi na Ufugaji Ili kuongeza thamani ya mazao yake na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza Pato la Taifa.
“Kuthibitisha namna tulivyodhamiria kuwainua kiuchumi wadau wa kilimo, NMB ndiyo benki ya kwanza nchini sio tu kukopesha kiasi kikubwa, bali pia kushusha riba kwa mikopo ya
kilimo, uvuvi na ufugaji hadi kufikia asilimia tisa, kwa mikopo hiyo inayoanzia sh. 200,000 hadi
sh. bilioni moja kwa mtu mmoja mmoja, vikundi, taasisi, mashirika na Vyama vya Ushirika vya Wakulima (AMCOS).
“Ndani ya miaka miwili hii, NMB tumetenga sh. Bil. 20 kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya mazao vijijini Ili kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao, ambako tayari zaidi ya sh. bilioni saba kati ya hizo zimeshakopeshwa ndani ya mwaka huu pekee. Pia tumetenga sh. bilioni 20 kuwezesha Program ya BBT, na mchakato wa kukamilisha hilo unaendelea baina yetu na Wizara ya Kilimo,”amesema Chilongola.
Chilongola amewapongeza wakulima wa parachichi, kahawa, mpunga na mahindi Mkoa wa Mbeya kwa kufungua zaidi
ya akaunti 87,044 ambazo ni kati ya akaunti 644,034 zilizofunguliwa na wakulima wote nchini katika kipindi cha miaka miwili.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato