Na Aveline Kitomary,TimesMajira online ,Dar es Salaam.
MATUMIZI ya barakoa yamekuwa maarufu sana hivi karibuni kutokana na mlipuko wa janga la virusi vya Corona.
Sehemu mbalimbali za maingilio ya watu hasa hospitali kumekuwa na uuzaji wa barakoa kutokana na ulazima wa kuivaa wakati wa kuingia maeneo hayo.
Lakini je ni nani ana majibu sahihi kuhusu usalama,ufanisi na usafi wa barakoa hizo?.
Wauzaji wa barakoa wanasema huwa wanazinunua kutoka katika maduka mbalimbali ya vifaa tiba na zingine zinashonwa kwa kutumia vitambaa.
Utunzaji wake huwa mikononi mwao kwa wakati huo huku wakiamini kuwa bidhaa wanazouza ni salama kwa matumizi ya wateja wao.
Ulinzi wa afya ya jamii ni jukumu la kila mtu lakini pia kuna Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa,Vifaa Tiba na Vitendanishi nchini(TMDA).
Mamlaka hii inajukumu la kuhakikisha kuwa kila bidhaa inayoingia sokoni inakidhi vigezo vinavyotakiwa ili kulinda afya ya jamii.
Moja ya bidhaa inayopimwa katika maabara za TMDA ni barakoa.
Utaratibu wa upimaji hupitia hatua mbalimbali ili kuweza kubaini ubora,ufanisi na usalama wake kwa matumizi ya wananchi na sio barakoa tu kuna dawa na vifaa tiba vingine.
Kuna njia mbalimbali zinazotumika kupima na kuhakiki ubora na usalama wa barakoa.
katika mamlaka yaani TMDA wao wanatumia njia mahususi ya uchunguzi kupitia taaluma ya ‘maikrobaolojia’ kitaalamu inaitwa “Bakterial filtration efficiency (BFE).
Uchunguzi huo hufanyika katika maabara kwa uangalifu mkubwa sana.
Maikrobaolojia ni Sayansi inayosomwa kwaajili ya kuweza kutambua viumbe wadogo sana,ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuleta madhara kwa binadamu na viumbe wengine ama faida pia,.
Viumbe vidogo hao kama ni vile bakteria,virusi na fangasi si rahisi kuweza kuviona kwa macho ya kawaida, ila kwa kutumia kifaa maalumu kinachojulikana kama darubini.
Viumbe hivi vidogo (micro-organism) vinaweza kuishi sehemu yoyote Ulimwenguni,licha ya kuwa na madhara wakati mwingine lakini pia huwa uwepo wake ni muhimu kulingana na mazingira husika.
Katika maabara ya TMDA pia hufanyika kipimo kinachojulikana kama “disinfectant challenge test” kwa ajili ya kupima ubora wa vipukusi vinavyotumika sambamba na barakoa katika kipindi cha hivi karibuni ili kupambana na janga ka Virusi vya korona.
SAMPULI ZA BARAKOA
Katika maabara ya TMDA iliyopo jijini Dar es Salaam upimaji wa sampuli za barakoa hufanyika kwa kila toleo linaloingia sokoni ama kuingizwa nchini.
Katika uchunguzi huu barakoa zinazotengenezwa au kuingizwa kutoka nje ya nchi hupitia hatua za upimaji katika nyanja ya maikrobaolojia.
Afisa mchunguzi wa TMDA, Obson Mkeya anasema katika maabara ya Maikrobaolojia wanahakikisha kuwa wanalinda afya ya jamii kwa kuchunguza kuchunguza bidhaa zote zinazodhibitiwa na mamlaka.
“Tunachokifanya katika sehemu ya Maikrobaolojia ni kuchunguza sampuli za dawa ,vifaa tiba na vitendanishi, tuna njia mbalimbali za kiuchunguzi tunafanya katika sampuli ikiwemo barakoa.
“Katika kuchunguza barakoa tunaangalia uchafuzi wa barakoa katika kiwango cha bakteria (bioburden), uchafuzi wa virusi vya korona na pia tunafanya kipimo cha uwezo wa barakoa endapo mtu akikohoa au kutoa/ kupokea hewa, je kile ambacho anakikohoa barakoa itaweza kumlinda mtu mmoja na mwingine? .
“Hivyo basi tunapima ubora ikiwa mtu akivuta au kukohoa itaweza kukinga kutokuenea kwa maambukizi,dira ni muhimu sana katika kutekeleza majukumu haya ya kila siku, kwa kuwa tumejikita katika kulinda afya ya jamii .
“Tukizungumzia vifaa tiba sio barakoa pekee yake, hivi ni aina mbalimbali ya visaidizi katika kusaidia hatua za matibabu; mfano sindano, vifaa vya kutolea na kuwekea damu na maji mwilini,na visaidizi vinginevyo kama “catheter” kwa kuweka uelewa wa pamoja vifaa vinavyotumika katika hatua za matibabu na vinavyomsaidia mgonjwa au muhitaji kwa ujumla wake hujulikana kama “vifaa tiba” anabainisha Mkeya.
Pia,anasema hawaangalii uchafuzi tu wa vifaa tu,bali hata mahusiano ya vifaa husika na mtumiaji yakoje,
“Mfano unaweza kuletewa vifaa tiba ambavyo ukitumia kwenye ngozi tu inasababisha madhara hivyo lazima tuhakikishe kemikali zinazotumika na malighafi zinazotumiwa kutengeneza vifaa tiba hivyo zinaweza kuhusiana na mtu ili aweze kupona bila madhara yoyote.
“Na katika maikrobaolojia pia tunaangalia uwepo wa viwango fulani wa vimelea katika baadhi ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi kwa njia ya uchunguzi kitalaamu inayoitwa “Microbial bioburden testing” mfano ukitaka kuangali uchafu wa barakoa ambayo imeandaliwa katika mazingira ambayo ya kawaida tarajia kukutana na kiwango fulani cha vimelea.
“Hivyo bhasi lazima tujihakikishie uwepo wa kiwango kisichozidi kiwango takwa husika,endapo uchunguzi ukabaini kiwango kimevuka nje ya takwa la ubora,utaratibu wa kitaasisi utafuatwa kuona namna nzuri na ya haraka ya kuweza kutoruhusu matumizi ya dawa au kifaa tiba hicho kutokuwepo sokoni “anaeleza Mkeya”
Anakazia kwa barakoa wanaangalia kiwango cha uchafuzi wa bakteria na uwezekano wa uchafuzi kwa kiwango cha virusi.
“Mfano sasa hivi tunazungumzia Covid 19,kwa maagizo ya Serikali barakoa zote ili ziweze kuingia nchini au kuuzwa kwa wananchi ni lazima kuangalia uwezekano wa uchafuzi wa virusi vya Corona.
HATUA ZA UCHUNGUZI
Mkeya anasema hatua ya kwanza katika kuchunguza barakoa ni kuandaa mahitaji kama vile ‘culture media na reagents zitakazotumika kulingana na njia ya uchunguzi (test method) atakayotumia mchunguzi.
Kwa kila riajenti inayotumika kupima vifaa tiba ‘Culture Media’ ‘kila mtengenezaji ameandika namna ya kuiandaa hivyo maelekezo yanatakiwa kufuatwa.
Hatua hii ya kwanza huanza baada ya meneja husika kupitia Mfumo wa Maabara (LIMS) kumgawia (issue) afisa mchunguzi ili majaribio ya kiuchunguzi yafanyike.
“Hatua za uchunguzi ni kufanya maandalizi ya vifaa vitakavyomsaidia kuchunguza,katika kuandaa vifaa ni lazima pia kupima uzito wa “culture media” husika halafu pH baada ya hapo anafanya utaratibu wa kuvitakasa (sterlization) .
“Sehemu ya utakasaji imetengwa mahususi inaitwa ‘autoclaving roo’ baada ya kumalizika kwa hatua ya usakinishaji,zinapelekwa maabara na hapo kipimo anachotaka kufanya kinaanza kufanyika mmoja wapo ni “BFE”.
“Kwa uchunguzi wa barakoa Media zinazotumika ni pamoja na TSA na SDA, Halafu anaweza akafanya kuangalia uwezekano wa kuambukiza virusi vya korona (Covid 19).
Mtaalamu huyo anasema hatua inayofuata ni uchakataji wa sampuli ikiwa ni pamoja na kupima BFE kuna mashine maalumu yaani (vacuum filtration pump manfold set).
“Kama tunatakiwa kufanya kipimo cha “bioburden” tunatumia miongozo mojawapo ikiwemo vitabu rejeo upande wa dawa na vifaa tiba,kama kuna uhitaji wa kufanya kipimo cha uchafuzi wa virusi tunatumia njia za kisasa zaidi za kimolekyula, mojawapo ya njia hiyo inaitwa Polymerize Chain Reaction (PCR),
Hatua ifuatayo ni kwa kufanya uoteshwaji katika mashine mahususi “incubator”kwa bakteria huwa ni saa 72,katika nyuzijoto 37.
“Na kukiwepo na wadudu( micro-organism) walioota huwa tunahesabu vimelea hivyo tayari kwa kufanya tathmini ya ubora kwa “kurejea miongozo anafafanua Bwana Mkeya.
MAIKROBAOLOJIA YA DAWA
Kwa upande wa dawa kuna aina tofauti tofauti za chunguzi zinazoweza kufanyika kulingana na dawa.
Mkeya anasema kuna dawa ambazo unaweza kuandaa katika mazingira ya kawaida hivyo kuwa na baadhi ya bakteria lakini kuna dawa ambazo hairuhusiwi mdudu aina ya bakteria kupatikana kwenye dawa.
“Ni kwa sababu hii dawa zinaingia mwilini moja kwa moja kupitia mishipa au misuli ya mwili, kimaikrobaolojia takwa lake ni kwamba hazitakiwi kupatikana na mdudu wa aina yoyote.
“Mtengenezaji kutokana na kiwango cha utengenezaji anatakiwa aseme ametengeneza katika mazingira safi na salama na rafiki kwa mtumiaji lakini sisi kama taasisi lazima kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kujiridhisha na usalama wa maandalio ya dawa hizo, na hivyo ili kuimarisha dhima na dira ya taasisi ya kulinda afya ya jamii lazima kufanya mlinganyo sahihi ni kuthibitisha kama inafanana na kile alichokisema yeye mtengenezaji.
“Tunachunguza tukiona ina uchafuzi wa kimaikrobaolojia tunaijulishana kimamlaka ili utaratibu stahiki wa kuziondoa ama kusimamishwa kuingia sokoni ufanyike haraka iwezekanavyo,”anaeleza Mkeya.
TUNAPIMA BARAKOA ZOTE
Meneja Mawasiliano wa TMDA, Gaudensia Simwanza anasema mamlaka hiyo inapima barakoa zote zinazoingia ama kuzalishwa hapa nchini na wazawa ili kuhakikisha zinaweza kuzuia maambukizi.
“Barakoa zote kuanzia zile zinazoingizwa ndani ya nchi,zile zinazotengenezwa ndani na hata zile ambazo zinashonywa kwa kutumia kitambaa tunapima kuangali kama zinakidhi vigezo vya kuingia soko.
“Endapo ukaguzi wetu ukibani kuwa bidhaa iliyopo sokoni haikidhi vigezo kwa kuchafuliwa tunaitoa mara moja tuko makini kulinda afya ya jamii kila wakati,”anafafanua Simwanza.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika