Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MBUNGE wa Jimbo la Tabora Kaskazini lililoko Wilayani Uyui Mkoani Tabora Almas Maige (Yaya Kwibyeda) amegawa majiko 300 ya gesi ya kupikia kwa wapiga kura wake jimboni humo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kugawa majiko hayo iliyofanyika jana katika Kituo cha Radio Uyui kinachomilikiwa na Mbunge huyo amesema kwa awamu hii ya kwanza anagawa majiko hayo kwa Viongozi wa Chama na Jumuiya zake.
Alibainisha kuwa Viongozi hao ni wa kata zote 19 zilizopo katika Jimbo hilo na awamu ya pili atagawa majiko yapatayo 500 kwa wapiga kura wake.
Mheshimiwa Maige alifafanua kuwa amegawa mitungi hiyo ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua mama kuni kichwani na kulinda mazingira.
Awali akitoa salamu za Chama katika hafla hiyo Katibu wa CCM Wilayani humo Bakari Mfaume alisema kugawa mitungi ya gesi ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama hicho ambayo inasizitiza suala la kulinda mazingira na kuwaondolea kero akinamama ya kubeba kuni kichwani.
Alitoa wito kwa Wataalamu wa halmashauri ya wilaya hiyo kutoa elimu ya manufaa ya matumizi ya gesi na madhara ya kutumia kuni na mkaa katika uhifadhi wa mazingira.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilayani humo Lubasha Makoba alimpongeza Mbunge kwa ubunifu wake mkubwa katika kuwatumikia wanaCCM na wakazi wote wa Jimbo hilo.
Alibainisha kuwa awali aligawa mifuko 30 ya saruji kwa kila kata kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Chama za kata na sasa amewaletea gesi ya kupikia ili kuwaondolea adha ya matumizi ya kuni na mkaa wakati wa kupika hali ambayo imekuwa ikichochea uharibifu wa mazingira.
Alisisitiza kuwa mbunge ana dhamira njema ya kuinua maisha ya wakazi wa Jimbo lake, kuepusha uharibifu wa mazingira na kulinda vyanzo vya maji hivyo akawataka waliopata majiko hayo kuyatumia vizuri na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Neema Mfugale alimpongeza Mbunge kwa kugawa mitungi hiyo na kusisitiza kuwa ametekeleza mpango wa serikali wa kudhibiti ukataji miti ovyo ambao huchochea uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa