March 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi,Child Support watoa msaada shule Jumuishi

Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Rungwe

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameungana na Mkurugenzi Mtendaji wa Child Support Tanzania (CST), Noela Msuya, kutoa msaada wa viti mwendo pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika Shule Jumuishi ya Katumba iliyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Mahundi ameungana na CST Machi 10, 2026 alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu ya shule hiyo pamoja na kukutana na watoto wenye ulemavu wanaotoka mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza katika ziara hiyo Mahundi amesema juhudi zinazofanywa na Noela Msuya kupitia taasisi ya Child Support Tanzania zinapaswa kuigwa na wadau wengine ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata huduma na haki sawa bila kubaguliwa.

“Nakupongeza sana Noela kwa namna unavyojitolea kuwagusa watoto wenye mahitaji maalumu. Unachokifanya ni jambo la ibada na ni mfano wa kuigwa. Kulea na kuwasaidia watoto wenye ulemavu ni baraka kubwa sana,” amesema.

Ameongeza kuwa wadau mbalimbali wanapaswa kujifunza kupitia juhudi za Noela Msuya kwani Serikali pekee haiwezi kutatua changamoto zote zinazowakabili watoto wenye ulemavu.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Child Support Tanzania, Noela Msuya, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kukarabati miundombinu ya shule hiyo ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu.

“Kupitia Child Support Tanzania tumekarabati miundombinu ya shule ili kuwasaidia watoto wetu kusoma katika mazingira rafiki bila vikwazo,” amesema Msuya .

Aidha Msuya ameongeza kuwa taasisi hiyo pia imetoa zaidi ya viti mwendo kumi, mafuta kwa watoto wenye ualbino, mafunzo kwa walimu, pamoja na kuanzisha klabu za ulinzi kwa watoto na klabu za wazazi.

Aidha, amesema wamekabidhi vifaa maalumu vya kujifunzia kwa watoto wenye uoni hafifu pamoja na kuandaa mpango mkakati wa kusaidia watoto wenye ulemavu.

Katika ziara hiyo, Mahundi aliambatana na Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Zanzibar, Nassir Ally, ambaye alisema ameguswa na juhudi za Mahundi katika kuwahudumia makundi yenye uhitaji na ameahidi kurejea katika kituo hicho ili kujifunza zaidi namna wanavyohudumia watoto wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu, ameshukuru Child Support Tanzania kwa msaada huo akisema utasaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu shuleni hapo.

Shule ya Katumba ni shule jumuishi inayopokea watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu kutoka mikoa mbalimbali nchini.