November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakimu na Majaji waaswa kuzingatia maadili,kanuni na katiba ya nchi wakati wa uendeshaji mashauri

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

JAJI Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Gerson Mdemu amewataka Mahakimu na Majaji kuzingatia maadili,kanuni na katiba ya nchi wakati wa uendeshaji wa mashauri mbalimbali.

Ameyasema hayo leo Machi 31,2023 wakati akifungua mafunzo kwa Mahakimu na Majaji yaliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema,Viongozi hao wa Mahakama wanapaswa kuzingatia mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kutoa haki katika kuzingatia misingi ya haki ambayo ipo katika katiba ya nchi.

Aidha amesema mafunzo hayo pia yatawaongezea weledi katika kuteleleza majukumu yao  .

“Amewaasa kuzingatia watakayofundishwa katika mafunzo hayo kwa sababu ndiyo yanayowajengea uwezo zaidi na kuwaongezea weledi zaidi katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa haki kama Mahakimu na Majaji kwa kuzingatia kanuni sharia na katiba ya nchi .”amesema Jaji

Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki  za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa amesema,katika mafunzo hayo Mahakimu na Majaji watapitishwa kwenye eneo la miiko ya kazi yao lakini pia wataangalia namna gani ya kuendesha mashauri yanatokana na uhuru wa kujieleza.

Vile vile amesema pia watapitishwa kwenye   masuala ya haki za wanahabari hapa nchini ili waweze kuendana na mabadiliko yanayoendelea kujitokeza lakini pia kutakuwa na mada kuhusu majukumu ya mahakama katika kuendesha au  kulinda haki za binadamu kwa kupitia mashauri ya kimkakati .

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (JMAT) Mary Kalomo amesema chama hicho kinaamini hiyo ni njia shirikishi kwa maana ya kushirikiana na wadau katika kuhakikisha wanaboresha katika eneo la upatikanaji haki za wananchi.

“Mafunzo haya yamejikita kwenye suala zima la maadili pamoja na kushughulika na mashauri yenye maslahi kwa umma.”