Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
RAIS John Magufuli, amekwenda kutoa pole kwa familia ya Balozi Mstaafu Job Lusinde aliyefariki dunia Julai 7,mwaka huu. Msiba wa Balozi Mstaafu Lusinde upo nyumbani kwake Kilimani Jijini Dodoma.
Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alikwenda nyumbani hapo akitokea Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambako ameongoza Kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama na Kikao cha Kamati Kuu ya CCM.
Akiwa nyumbani kwa Marehemu Balozi Mstaafu Lusinde, Rais Magufuli alikutana na Mjane wa Marehemu, Sara Lusinde, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu ambapo ameeleza kuguswa na kifo cha Balozi Mstaafu Lusinde na kwamba daima atamkumbuka kwa mchango wake alioutoa akiwa Waziri wa Ujenzi, ushauri wake mzuri na moyo wake wa upendo na ukweli.
Rais Magufuli ameeleza kuwa wakati wa utumishi wake Balozi Mstaafu Lusinde alikuwa mzalendo wa kweli, mchapakazi na aliyetetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi, na kwamba hata alipostaafu aliisemea vizuri Dodoma.
Amewataka wafiwa wote kuwa wastahimilivu na kumpuzisha salama hapo leo atakapozikwa.
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme