December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafanikio ya TANAPA katika miaka mitatu Serikali ya Awamu ya Sita

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

UNAPAZUNGUMZIA Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ni Taasisi ya Umma ambayo lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa.

Maeneo ya Hifadhi za Taifa yanawakilisha kiwango cha juu cha uhifadhi wa wanyamapori nchini (highest conservation status of wildlife), ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoruhusiwa kufanyika.

Hadi sasa Shirika hilo linasimamia Hifadhi za Taifa 21, zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na 10.2% ya eneo lote la nchi.

Tanzania imekuwa ikijitahidi sana katika kuendeleza sekta ya utalii na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imekuwa ikicheza jukumu muhimu katika kufanikisha lengo hili.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, TANAPA imepata mafanikio makubwa ambayo yamechangia sana katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

Akizungumzia mafanikio ya TANAPA, chini utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita ambaoyo inaongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji anasema mafanikio hayo ni jitihada za makusudi zinazoendelea kufanywa na Rais huyo.

Kamishna Kuji anasema, ushiriki wa Dkt. Samia katika kukuza sekta ya uhifadhi wa wanyamapori na utalii ikiwemo ushiriki wake kwenye filamu maarufu ijulikanayo kama “Tanzania: The Royal Tour” ndio chanzo cha mafanikio ya TANAPA kupiga hatua.

Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji

Anasema, filamu hiyo imeleta chachu kubwa katika ukuaji wa utalii hapa nchini. anampongezwa sana Rais kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii hapa nchini, pamoja na kuendelea kuelekeza fedha katika sekta ya uhifadhi na utalii.

Ametaja miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na;-

KUONGEZEKA KWA IDADI YA WATALII

Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji anasema Filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” ilifungua
milango ya utalii na fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa hasa baada ya nchi kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19.

Hata hivyo anasema,TANAPA imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa nchini.

Anasema, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, kuhakikisha usalama wa wageni, na kutekeleza mikakati ya masoko ya kimataifa. Matokeo yake, Tanzania imeendelea kuwa moja ya vivutio vya utalii barani Afrika.

“Kuongezeka kwa idadi ya watalii Katika Hifadhi za Taifa kumekuwa na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa mwaka hadi mwaka.

“Katika mwaka 2018/2019 jumla ya Watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa walikuwa watalii 1,452,345 ikihusisha watalii wa ndani (719,172) na nje (733,173),” anasema Kamishna Kuji.

Hata hivyo anasema, idadi hiyo ilianza kupungua mwanzoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga ya UVIKO-19 na kusababisha idadi ya wageni kupungua hadi kufikia watalii 485,827 katika
mwaka 2020/2021.

Kufuatia anguko hilo, Kamishna Kuji anasema Serikali ya awamu ya sita (6), ilichukua hatua mbalimbali katika kurejesha hali ya utalii kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo kutengenezwa kwa miongozo maalum (Standard Operating procedures – SOPs) ya kupokea na kuhudumia watalii, na pia kuruhusu upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19.

Anasema, kutokana na jitihada hizo za Rais, mnamo mwaka 2021/2022 idadi ya watalii ilianza kupanda na kufikia watalii 997,873. Hali ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda ambapo mwaka 2022/2023 idadi ya watalii waliongezeka na kufikia 1,670,437.

Aidha, anasema kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 – Machi 19, 2024 idadi ya watalii 1,514,726 (wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183) ambao wametembelea Hifadhi za Taifa, sawa na ongezeko la asilimia 5 ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 (wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676) katika kipindi husika.

Anasema, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka
wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667).

Vilevile, katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024. Ongezeko hili limechangia ongezeko la mapato.

Mbali na hivyo pia, anasema kuongezeka kwa Mapato Katika kipindi cha miaka mitatu, kumekuwepo na ongezeko la kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023) sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024) Shirika limekusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811,506 mpaka Machi 2024.

“Kiasi hicho cha (Bilion 340) ni ongezeko la shilingi 44,634,296,959 ambayo ni sawa na asilimia 15. Shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha shilingi 382,307,977,497 hadi Juni 2024.

“Mapato hayo ya sasa yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO – 19 ambayo
yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika Shirika,” anasema Kamishna huyo.

Pia, anasema Ongezeko hilo la watalii na mapato linaenda sambamba na malengo ya Ilani ya Chama Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini kufikia milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani Bilioni 6 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Katika hatua nyingine Kamishna Kuji anasema, mafanikio mengine ambayo TANAPA imeyapata katika kipindi cha awamu ya sita ni;

“Kuongezeka kwa masoko mapya ya Utalii.
Kumekuwepo na kuchipuka kwa masoko mapya ya utalii yenye idadi kubwa ya watalii ambapo inatoa uhakika wa kuendelea kupokea watalii wengi kuja kutembelea Hifadhi za Taifa.

“Masoko haya mapya ni pamoja na China, Urusi,
Ukraine, Poland, Jamhuri ya Czech na Israeli,” anasema.

Lakini pia, anasema kutambulika Kimataifa, TANAPA imefanikiwa kupata tuzo ijulikanayo kama “Best Practice Award” ambayo hutolewa kila mwaka na taasisi ya “European Society for Quality Research – ESQR”.

Anasema Tuzo hiyo ya utoaji wa huduma bora kimataifa hutolewa na taasisi hiyo baada ya kutambua taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za ubora wa viwango vya hali ya juu kimataifa.

Vilevile anasema, TANAPA imeendelea kupata tuzo zinazotolewa na taasisi ya ESQR kwa kipindi cha miaka minne (4) mfululizo ambazo kati ya hizo, tuzo za miaka mitatu (3) mfululizo zimepatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango cha “Platinum category” mwaka 2021, “Gold category” mwaka 2022 na “Diamond category” mwaka 2023.

“Hifadhi ya Taifa Serengeti imepata tuzo itolewayo na shirika la “World Travel
Awards (WTA)” ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo
(2019 hadi 2023).

“Tuzo tatu (3) kati ya hizo tano (5) zimepatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita (tuzo za mwaka 2021 hadi 2023),” anasema Kamisha Kuji.

Aidha, anasema Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Kilimanjaro zilipata tuzo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2021 na 2022 ya kuwa vituo vyenye mvuto katika utalii (best of the best outdoor enthusiasts). Tuzo hizo hutolewa na jukwaa la kimataifa lijulikanalo kwa jina la “Trip Advisor”.

Pia, anasema kampuni ya Explore Worldwide yenye makao yake makuu nchini Uingereza mwaka huu imeutambua Mlima Kilimanjaro kuwa
namba moja ya Alama za Asili za kudumu na zinazokumbukwa zaidi ulimwenguni (World’s topmost unforgettable natural landmarks).

Anasema, tuzo hizo zimeliongezea Shirika kuaminiwa na wateja mbalimbali na kutoa uhakika kwao kuhusu aina ya huduma zitolewazo, kutambulika zaidi na kuongeza idadi ya watalii pamoja na kutoa uhakika kwa watalii na wadau wa utalii kuhusu ubora wa hifadhi.

UWEKEZAJI KATIKA MIUNDOMBINU YA UTALII

Akizungumzia uwekezaji katika miundombinu ya Utalii, Kamishna huyo wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji anasema katika kipindi cha miaka mitatu, TANAPA imefanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha miundombinu ya utalii kama vile barabara, madaraja, na huduma za malazi.

Anasema,TANAPA imeendelea kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kukamilisha ujenzi wa lango la kisasa la Naabi lenye uwezo wa kupokea zaidi ya magari 600 na wastani wa wageni zaidi ya 1,500 kwa siku.

Pia, anasema kuimarishwa kwa Miundombinu, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Ujerumani (KfW), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), imeendelea kuboresha (kujenga na kukarabati) miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vilivyopo katika Hifadhi za Taifa.

Aidha, anasema shirika lina mtandao wa barabara ambao umeongezeka kutoka urefu wa kilometa 7,638 mwaka 2021 na kufikia urefu wa kilometa 16,471 mwaka 2024. Kazi nyingine za miundombinu zilizofanyika ni pamoja na:-

“Kukarabati wastani wa kilometa 3,938 za Barabara. Kutengeneza njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 334. Ujenzi wa madaraja 14 na vivuko 399.

“Kukarabati viwanja vya ndege (Airstrips) 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) na viungio vyake pamoja na
maegesho ya ndege kwa kiwango cha changarawe katika hifadhi za Serengeti (1), Nyerere (3), Tarangire (1), Mkomazi (2), Saadani (1),
Mikumi (1) na Ruaha (2).

“Viwanja vya kutua helikopta (helipads)
(5) katika Mlima Kilimanjaro vilijengwa kwa kiwango cha zege kwa kuzingatia kanuni za TCAA na ICAO.

“Kununua mitambo 59 ya aina mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Dunia (Mradi wa REGROW) na IMF (Mradi wa
TCRP),” anasema Kamishna Kuji.

Mbali na hivyo pia, anasema Mitambo iliyonunuliwa kupitia mradi wa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii kusini mwa Tanzania (Resilient Natural Resources Management for Tourism and Growth – REGROW) ni motor grader 5, compactor 3, low loader 2, malori 17, excavator 2, bulldozers 2, concrete mixers 5, matrekta 7, malori ya kubebea maji 5.

Anasema, Magari ya sinema (cinema vans) 4, magari ya kutolea elimu kwa wanafunzi na jamii “expedition trucks” 3 na malori ya kutengenezea magari (mobile workshop)

  1. Jumla ya shilingi 27,873,761,395.00 zilitumika kununua mitambo hiyo.

Vilevile anasema, Mitambo iliyonunuliwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TCRP) ni motor grader 5, compactor 4, low loader 4, malori 15, excavator 4, magari madogo 7 (Landcruiser).

Concrete mixer 1, Back low loader 1 na malori ya kubebea maji 4) vyenye thamani ya shilingi 17,765,532,026 zilitumika kununua mitambo hiyo. Mitambo hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya barabara katika Hifadhi zetu.

Anasema, katika kipindi cha miaka mitatu TANAPA pia imeweza kujenga malango mapya 10 na ya kisasa katika Hifadhi za Taifa Tarangire (2), Mkomazi (3), Serengeti (2) na Nyerere (3).

KUKUZA USHIRIKIANO NA WADAU WA UTALII

Kamishna Kuji amezungumzia pia, kukuza ushirikiano na wadau wa Utalii, ambapo anasema TANAPA imeendeleza ushirikiano na wadau wa utalii ikiwa ni pamoja na makampuni ya utalii, taasisi za elimu, na mashirika ya kimataifa.

Anasema, hatua hiyo imeongeza ufahamu wa kimataifa kuhusu vivutio vya utalii vya Tanzania na kusaidia katika uendelezaji wa sekta hiyo muhimu kiuchumi.

Hata hivyo anasema, kuongezeka kwa wigo wa shughuli za utalii wa puto (balloon) kutoka kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa hifadhi ya Mikumi;

“Utalii wa faru (Hifadhi ya Taifa Mkomazi), utalii wa baiskeli (Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha);

“Utalii wa michezo na burudani (Hifadhi ya Taifa Serengeti – Mchezo wa tennis na Hifadhi ya Taifa Mikumi – Mpira wa miguu, pete na kikapu),” anasema.

Pia, anasema ongezeko kwa mbio za Marathon katika maeneo ya ndani na pembezoni mwa hifadhi za Taifa, zimekuwa zikivutia washiriki wengi na wakati huo huo kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo husika.

Anasema, Hifadhi zilizofanikiwa kuratibu mbio za Marathoni ni pamoja na Hifadhi ya Taifa
Serengeti, Arusha, Mkomazi, Ruaha, Katavi, Mahale, Gombe, Burigi￾Chato na Kilimanjaro.

KUIMARISHA UHIFADHI WA MALIASILI

Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), anasema Mamlaka imeendelea kutekeleza mikakati thabiti ya uhifadhi wa maliasili ikiwa ni pamoja na kupambana na ujangili, kuhifadhi mazingira asilia, na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi.

Kamishna Kuji anasema, Serikali ya awamu ya sita (6) imeweka mazingira wezeshi kwa Shirika kusimamia maliasili zilizopo katika Hifadhi za
Taifa hapa nchini.

Anasema, Mazingira wezeshi ni pamoja na upatikanaji wa rasimilimali fedha, rasilimali watu na vitendea kazi kama magari, mitambo ya kutengeneza barabara na mafunzo kwa watendaji. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni
pamoja na:

i. Kudhibiti uwindaji wa wanyama adimu ambapo hakukuwa na tukio la kuuawa kwa Faru, Sokwe au Mbwa mwitu.

ii. Kupungua kwa matukio ya uwindaji wa tembo kutoka matukio 4 kwa mwaka 2021/2022 hadi matukio mawili (2) kufikia Machi 2024.

iii. Kukamata silaha mbalimbali 274 (shot gun 13, Assault Riffles-7 (SMG, SAR na AK 47), Riffle – 7 (.458, .404, .375, 30-06), magobore 245 pamoja na kutegua nyaya 48,665.

iv. Kudhibiti uingizwaji wa mifugo hifadhini kwa kufanya doria na kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazoishi jirani na hifadhi.

Aidha, anasema madhara ya uingizaji wa mifugo ni pamoja na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji, maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama wafugwao kwenda kwa wanyamapori, kuendelea kushamiri na kusambaa kwa mimea vamizi na kuharibu shughuli za utalii.

V. Lakini pia kusimamia na kuendesha mashauri katika mahakama mbalimbali hapa nchini dhidi ya wahalifu waliokamatwa. Jumla ya mashauri 4,831 yalitolewa maamuzi kati ya mashauri 4,978 yalifunguliwa na kusikilizwa.

Anasema, hiyo imechangia sana katika kulinda viumbe hai na maliasili za Tanzania kwa vizazi vijavyo.

KUKUZA AJIRA, KIPATO KWA JAMII ZA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI ZA TAIFA

Akizungumzia kipato kwa jamii za vijiji vilivyozunguka hifadhi za Taifa, Kamishna Kuji anasema kupitia miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, TANAPA imechangia katika kukuza ajira na kipato kwa jamii za vijiji vinavyozunguka hifadhi za taifa.

Hiyo imeleta matokeo chanya kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo.

Anasema, Katika kipindi cha miaka mitatu, Shirika limeendelea kuboresha mahusiano na
jamii zilizo jirani na hifadhi za Taifa katika shughuli za uhifadhi na utalii. Kupitia
mashirikiano haya zimepatikana faida mbalimbali ikiwemo;

i. Kuibuliwa na Kutekelezwa kwa Miradi ya Kijamii “Support for Community Initiated Projects” (SCIPs). Katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya miradi 59 ya kijamii yenye thamani ya shilingi 30,785,819,981 ilitekelezwa.

Kamishna Kuji anasema miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 20, mabweni 2, nyumba 7 pacha za walimu, zahanati 12, nyumba pacha za wauguzi 6, miradi ya maji 6, barabara 5 zenye urefu wa kilomita 76 na bwalo la chakula kwa wanafunzi 1 na ununuzi wa madawati 680.

Aidha, anasema miradi hiyo imetekelezwa katika Wilaya za Ruangwa, Makete, Mbeya, Mbarali, Mpanda – Halmashauri ya Nsimbo, Uvinza, Kigoma, Muleba, Bariadi, Bunda, Serengeti, Mbulu, Arumeru, Rombo, Longido, Mwanga, Same, Korogwe, Lushoto, Pangani, Kilosa, Kilombero, Kilolo, Lindi na Ngorongoro (tarafa za Loliondo na Sale).

Vilevile anasema, ujenzi wa miradi hiyo umesaidia kupunguza kero kwa jamii na kuongeza usalama wa wanafunzi na kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya sambamba na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Hata hivyo anasema, miradi hiyo imesaidia kuimarisha mahusiano mazuri kati ya jamii na hifadhi na kuifanya jamii kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa Maliasili.

(ii). Utekelezwaji wa Miradi ya Uzalishaji Mali (TANAPA Income Generating Projects – TIGPs).

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya uzalishaji mali, Kamishna Kuji anasema jumla ya vikundi 138 vimewezeshwa miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, uchakataji wa viungo vya chakula na ufugaji.

Anasema, jumla ya shilingi billion 2.4 zilitumika kuwezesha miradi ya uzalishaji mali. Pia, Benki za Kijamii za Uhifadhi “Community Conservation Bank” (COCOBA) 159
zilianzishwa kupitia mradi wa REGROW na kupewa fedha mbegu kiasi cha shilingi 1,453,272,934.

Miradi hiyo imesaidia kuongeza wastani wa pato la wananchi katika maeneo husika na kupunguza utegemezi wa Maliasili.

iii. Kutolewa kwa Ufadhili wa Masomo kwa Wananchi Kupitia Mradi wa REGROW.

Kuhusu ufadhili wa masomo Kamishna Kuji anasema, Jumla ya wanafunzi 1,051 kutoka vijiji 60 vinavyotekeleza mradi wa REGROW wamepatiwa ufadhili wa masomo wenye thamani ya shilingi 4,273,315,700 katika vyuo mbalimbali vya kitaaluma hapa nchini.

Anasema, Ufadhili huo umesaidia kuongeza kiwango cha uelewa kwenye jamii na kuongeza uwezo wa uzalishaji mali kwenye jamii husika.

iv. Kuendelea Kuwezesha Uandaaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na Utoaji wa Hati za Kimila (Community Customary Right of
Occupancy – CCRO’s).

Akielezea hilo, Kamishna Kuji anasema TANAPA kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) na Shirika lisilo la kiserikali la “Frankfurt Zoological Society – FZS” imeendelea kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 57 vya wilaya za Serengeti, Morogoro, Kisarawe, Ulanga, Tunduru na Liwale na kutoa hati za kimila 16,243.

Anasema, Kati ya hati hizo, hati 9,874 zilitolewa kwa jamii kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Nyerere na hati 6,612 zilitolewa kwa jamii

Vilevile anasema, kutoka kwenye vijiji vilivyo katika wilaya ya Serengeti vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti. Hata hivyo wanaendelea kuandaa hati za kimila kwenye Wilaya za Bunda, Bariadi, Tarime, Meatu, Itilima na Busega.

Anasema, Uandaaji huo wa matumizi bora ya ardhi umesaidia kupunguza migogoro ya kimatumizi kati ya binadamu na wanyamapori kwenye maeneo husika na kuwajengea usalama katika umiliki wa ardhi kwa jamii zinazopakana na hifadhi.

KUELIMISHA JAMII KUHUSU UHIFADHI

Akizungumzia kuelimisha jamii kuhusu Uhifadhi, Kamishna huyo wa TANAPA anasema kumekuwepo na ongezeko la idadi ya wananchi wanaofikiwa na elimu ya uhifadhi kutoka wananchi 169,245 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia wananchi 211,986 katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Anasema, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Desemba 2023 wananchi 125,389 wamefikiwa na elimu ya uhifadhi.

Ongezeko hillo linatoa uhakika wa kuwa na wanajamii wanaoelewa masuala ya uhifadhi na hivyo kuongeza uhakika wa ushiriki wa wananchi kwenye uhifadhi na ulinzi wa maliasili.

CHANGAMOTO

Hata hivyo Kamishna Kuji amezungumzia jinsi Shirika hilo linavyokabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo: –

Mabadiliko ya tabia nchi; (ukame, mafuriko n.k), Uwepo wa mimea vamizi inayoathiri upatikanaji wa chakula na mizinguko ya wanyamapori.

Uwepo wa ujangili, Matukio ya uingizwaji wa mifugo ndani ya hifadhi, Matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya jamii.

Gharama kubwa za matengenezo ya miundombinu ya barabara kutokana na mvua nyingi (el-nino); na

Uchache wa miundombinu nje na ndani ya hifadhi za kusini, mashariki na magharibi mwa nchi unaosababisha wawekezaji wachache.

Kwa kumalizia, miaka mitatu ya mafanikio ya TANAPA katika serikali ya awamu ya sita imejaa mafanikio makubwa katika kuendeleza sekta ya utalii, kuhifadhi maliasili za asili, na kukuza maendeleo ya jamii za vijiji vinavyozunguka hifadhi za taifa.

Hata hivyo, changamoto bado zipo ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, ujangili, na usimamizi endelevu wa rasilimali za utalii.

Ni muhimu kwa TANAPA kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa mafanikio haya yanadumu na yanawanufaisha Watanzania wote.

Kamishna Kuji amewahakikishia kuwa, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), litataendelea kusimamia jukumu la kuhifadhi maliasili zote na kutunzwa kikamilifu wakati wote.

Ulinzi wa malisili, usalama wa watalii, usalama wa watumishi wa TANAPA, na usalama wa wawekezaji utaendelea kuimarishwa wakati wote ili kuhakikisha kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania zinaendelea kuwa ni maeneo salama na sahihi kwa watalii na wawekezaji.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika maeneo yaliyoainishwa katika Hifadhi za Taifa kwa nia ya kuboresha huduma za malazi kwa wageni.

Ametoa wito kwa watanzania kutembelea hifadhi zetu kwa ajili ya kujivinjari na kupumzika.

Uboreshaji huo wa kutembelea hifadhi utawezesha Serikali kufikisha watalii milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.