Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
WIZARA ya Madini kupitia Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo ya uchimbaji wa madini kwa ajili ya Wachimbaji wadogo wa Madini nchini ambapo sehemu kubwa inalenga Vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 45.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 16,2026 na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini Mhandisi Hamisi Kamando wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa miradi ya maendeleo na fursa za vijana katika sekta ya Madini 2025/26 ambapo amesema hadi sasa jumla ya maeneo 65 yamependekezwa kutengwa kwa ajili ya kugawiwa kwa Wachimbaji Wadogo katika mikoa ya kimadini ya Mtwara, Manyara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani, Tanga, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya na Ruvuma.
“Sekta ya Madini ni moja ya sekta za kimageuzi katika uchumi inayosaidia katika kukuza na kuchagiza maendeleo katika sekta zingine na kuwezesha wananchi wake hasa vijana kunufaika na rasilimali madini. Katika kuhakikisha sekta hii inawanufaisha wananchi hususan kundi la vijana, Serikali ya awamu ya sita kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2025 imeweka vipaumbele vyake na sekta ya madini vinavyolenga kuwawezesha vijana katika ajira, kukuza ujuzi wa kisayansi na uwekezaji,”amesema.

Mha.Kamando ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo wa madini, kuwapatia leseni na kuwaendeleza.Kuifanya Tanzania kuwa kituo cha uuzaji wa madini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuimarisha masoko ya madini na vito ikiwamo Tanzanite kwa kujenga jengo la Tanzanite Exchange Centre (TEC) katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro.
Aidha ametaja kipaumbele kingine ni kuhamasisha na kusimamia shughuli za uongezaji thamani ya madini nchini na kutokana na umuhimu na nafasi yake katika kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla, Serikali itaweka mazingira maalum ya kisera na kisheria yatakayohakikisha kuwa madini adimu na ya kimkakati (strategic mineral resources and rare earth elements) yanachimbwa kwa ubia na wawekezaji kutoka nje.

Pamoja na hayo amesema Tume itahakikisha madini yote yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa Kituo Kikuu cha Uuzaji wa Madini katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
“ Serikali itaweka sera, sheria na kanuni zitakazohakikisha kuwa madini haya hayasafirishwi nje bila kuongezewa thamani nchini,”amesisitiza.


More Stories
Serikali kuweka uzio wa umeme kudhibiti Tembo hifadhi ya Lwafi
Diwani Bhojani atoa nguo kwa watoto Ilala
Kutoka ndoto hadi furaha,umeme kumfikia Sesilia