December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maelekezo ya Rais Dkt. Samia Kongamano la Utalii yatimia

Na Mwandishi WetuTimemajiraonline, Arusha

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amefungua rasmi kongamano la uwekezaji kwenye Sekta ya utalii mkoani Arusha lenye kauli mbiu isemayo;

“Uwekezaji katika Utalii Endelevu: Changamkia Fursa za Uwekezaji baada ya Programu ya Tanzania-The Royal Tour”.

Kongamano hilo lenye lengo la kuboresha Sekta ya Utalii ni maelekezo mahususi ya Rais Samia, ambaye aliagiza Wizara ya Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili kukaa kwa pamoja na kuja na mikakati ya uwekezaji itakayoboresha sekta hiyo mkoani Arusha.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, alisema ni muhimu sekta binafsi na Serikali kushirikiana kwa kuhakikisha miundombinu bora katika maeneo ya hifadhi pamoja na huduma za malazi zilizoboreshwa ili kuvutia watalii wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, aliwahakikishia wadau wa utalii kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuitangaza nchi kimataifa, kuboresha miundombinu katika maeneo yenye vivutio vya utalii na kuboresha huduma katika mnyororo wa thamani wa shughuli za utalii na pia kuainisha vivutio maalum kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu Maliasili, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Mbaga Kida, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda, Viongozi Waandamizi wa Chama na Serikali pamoja na Wadau wa Uhifadhi na Utalii wa jijini Arusha.