November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani,wananchi Lushoto watakiwa kushiriki uchaguzi

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

MADIWANIu wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wametakiwa wao na wananchi wote kwenda kujiorodhesha kwenye maeneo yao kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ikupa Mwasyoge kwenye Baraza la Madiwani, na kuongeza kuwa zoezi la kujiorodhesha kwenye maeneo yao litafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024.

Lakini pia amewakumbusha viongozi wa vijiji na vitongoji, mwisho wa kuhudumu kwenye Ofisi za Serikali za Vijiji ni Oktoba 25, mwaka huu, na hawatatakiwa kufanya chochote kwenye ofisi hizo, na itabidi waache mihuri ya Serikali ofisini, na wala hakuna barua yeyote itapokelewa kwa jambo lolote baada ya tarehe hiyo.

“Mnachotakiwa kukumbuka ni kwamba kuanzia Oktoba 11 hadi 20, kila mmoja kwenda kujiorodhesha kwenye eneo lake. Kama ni kwenye mtaa wako, kijiji chako au kitongoji chako tayari kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na hii ni muhimu sana. Lakini tukawahimize vijana wetu ambao yamkini uchaguzi uliopita walikuwa hawajatimiza miaka 18, lakini sasa wamefikisha miaka 18.

“Na wao wawe ni miongoni mwa watakaojitokeza kujiorodhesha ili waweze kupiga kura. Lakini na wale wenye sifa ya kugombea ni wenye umri wa miaka  21, wanatakiwa wajitokeze kwenda kugombea, kuna nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, kuna wale wajumbe wa Serikali ya Kijiji, pia kuna wajumbe wa kitongoji, na lakini pia tuna wajumbe wa viti maalumu kwa wanawake, maana katika uongozi, theluthi moja inatakiwa wajumbe wawe wanawake” amesema Mwasyoge.

Hivyo amewaasa madiwani kwenda kuwahimiza wanawake nao waweze kugombea nafasi ambazo zitaweza kutangazwa, na kuongeza kuwa maeneo ambayo uchaguzi utafanyika,  tangazo litatolewa Septemba 16, mwaka huu, na watu waendelee kufuatilia matukio ya uchaguzi huo, huku viongozi wa vijiji wakijua mwisho wa ukomo wa madaraka yao.

“Lakini kule katika maeneo yetu tuwakumbushe viongozi waliopo madarakani kuwa uongozi wao unakoma Oktoba 25, mwaka huu. Kuanzia Oktoba 25, 2024 hawataendelea kutekeleza majukumu mengine. Tarehe 26 au 27 hatutaona mihuri wala saini ambazo zimesainiwa na wao, na naomba sana hilo,  nilishawaelekeza watendaji kusimamia hilo na kufuatilia” amesema Mwasyoge.

Mwasyoge amesema mtu mwenye sifa ya kuchaguliwa ni lazima awe raia wa Tanzania, na anajua kusoma na kuandika, na anajua kuandika lugha ya Kiswahili ama Kingereza, na mgombea ni vizuri akawa mwenyeji wa eneo husika ili kukwepa watu kuanza kuweka mapingamizi.

Mwasyoge ameitaka jamii, pamoja na kuwaombea watoto waliofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba Septemba 11 na 12, ipo haja ya kuhakikisha watoto hao wanasubiri matokeo, na kuendelea na elimu ya sekondari badala ya kuwaruhusu watoto hao kwenda kufanya biashara ndogo ndogo mijini.

“Tuendelee kuwaombea watoto wetu waliofanya mtihani wa Taifa wa darasa la saba Septemba 11 na 12, huku tukimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye bado ameendelea kutoa nafasi yaani elimu bila malipo, kwamba watoto wanapomaliza darasa la saba wanaendelea kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne bila malipo.

“Hivyo niombe sana wote tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kwamba hawa vijana wanapomaliza hapo wasije wakatoka na kwenda kufanya shughuli nyingine, kwani uzoefu umeonesha maeneo mengine, mtoto akimaliza tu, anakwenda kutafuta ajira” amesema Mwasyoge.