Na Moses Ng’wat, Ileje.
WATAALAMU wa afya wilaya ya Ileje mkoani Songwe wameagizwa kuanza kutoa elimu ya matumizi sahihi ya kondomu za kike ili kukabiliana na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Ukimwi.
Agizo hilo limetolewa leo Januari 30,2024 wakati wa kikao cha baraza la madiwani robo ya pili katika halmashauri ya Ileje baada ya kuibuka kwa ajenda ya wanawake wilayani humo kuogopa kutumia kondomu kutokana na ukubwa wake.
Mwenyekiti wa kamati ya afya na ukimwi ambaye ni diwani wa kata ya Itale Fahari Mwampashi amesema hofu ya watumiaji wa kondomu hizo wanasema ukubwa ukilinganisha na maumbile yao wakitaka zipunguzwe ukubwa.
“Wanawake wanaogopa kuvaa hizo kondomu wakidai zitabakia ndani na kuhatarisha afya zao, huku wakiomba wataalamu wa afya kupitia ofisi ya mganga mkuu kuwekeza nguvu ya utoaji elimu,” amesema Mwampashi.
Vema Rungwe diwani viti maalumu amesema matumizi ya kondomu za kike ukubwa wake na uvaaji ni changamoto ,na kwamba hakuna msukumo wa kuzitangaza kwa jamii ili kuleta uelewa badala yake za kiume kupewa kipaumbele.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ubatizo Songa amesema kutokana na mkakati wa kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi, wataalamu wa afya endeleni kutoa elimu ya matumizi sahihi ya kondomu za kike na kiume ili jamii iwe na uelewa sahihi wa matumizi yake.
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya Ileje Joyce Ongati amekili kuwepo kwa changamoto ya matumizi ya kondomu za kike kwa wanawake licha ya elimu kutolewa na kuahidi kuendelea kuongeza juhudi za elimu zaidi.
Mmoja wa mwananchi akihojiana na gazeti hili Mariamu Shimwela amesema awali waliletewa kondomu hizo lakini wanaogopa kuzitumia kwa hofu ya maumbile yao kuwa madogo walikilinganisha na ukubwa wa kondomu zilivyotengenezwa.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu