October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani waomba wazee kurahisishiwa upokeaji fedha za TASAF

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbarali

BAADHI ya wazee wilayani Mbarali mkoani Mbeya wameiomba serikali kuwarahisishia upokeaji fedha za TASAF kwani mfumo uliopo kwa sasa kulingana na geographia ya wilaya hiyo kuwalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo .

Kauli hiyo imetolewa leo Diwani wa vitimaalum kata ya Ilongo ,Safihamidu Alma’s wakati akizungumza na Timesmajira amesema kuwa serikali imeendelea kutoa huduma kwa wananchi wenye hali ya chini kimaisha ambao wamekuwa wakinufaika na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF).

“Ni kweli fedha hizi zimeingia katika halmashauri yetu ya Mbarali kwa robo ya kwanza lakini kumekuwepo na mabadiliko ya utaratibu wa namna gani mnufaika anaweza kuzipata fedha ikiwemo huyu mnufaika fedha zake kuingia kwenye akaunti yake benki lakini kwa hili naamini serikali ilikuwa na nia njema lakini imeleta changamoto kubwa kwani huduma hii wengi wao ni wazee na wananchi ambao wapo vijiji vya ndani ambavyo hata huduma za kibenki hamna hivyo wamekuwa wakitembea zaidi ya kilometa saba kwa ajili ya kufuatilia huduma hiyo ili waweze kutoa fedha zao na wengi wao ni wazee”amesema .

Hata hivyo Diwani huyo ameiomba idara husika kufanya marekebisho madogo kuangalia ni wanufaika gani wenye kiwango gani ambao wanaweza kukabiliana na changamoto hiyo ,lakini pia waangalie umri kwa wazee ambao hawezi kutembea kilometa zaidi ya saba imekuwa ni mateso.

Jeremia Kisangai ni Diwani wa Kata ya Miyomboni ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ameiomba serikali kuwafikilia wazee hawa kwa kuwarudisha katika mfumo wa zamani wa upokeaji fedha ili kuweza kuwaondolea adha hiyo ya kuteseka kwa kutembea umbali mrefu.

Roman Kessy kaimu Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Mbarali amesema maboresho ya mfumo yanaendelea kufanyika kutokana na hitaji la mlengwa.

Amesema serikali imejitahidi kupunguza gharama na kuhakikisha wazee wanapata fedha kwa wakati lakini kulikuwa na uingizaji wa fedha taslimu, kwenye simu pamoja na benki na kwenye maeneo yenye shida kuna sehemu wanabadilisha wanaenda kwenye mfumo ambao wanaona ni rahisi kupatiwa huduma hiyo.

“Maboresho yanaendelea kufanyika kulingana na hitaji la mlengwa na mwisho kufika hatima na wengine kuishia benki au kupokelea kwenye simu lakini tunaamini changamoto hii itakwisha yote kulingana na maboresho yanayoendelea”amesema Kessy.

Mmoja wa wazee wa kata ya Mawindi Aman Juma amesema suala hilo limekuwa changamoto kwao kwani baadhi ya wazee wanatoka kata za mbali na kulingana na hali za uzee walionao inawabidi kushindwa kutembea.