Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kwa kauli moja, limebariki hoja ya kutaka Jimbo la Korogwe Vijijini kugawanywa na kuwa majimbo mawili ili kuweza kuongeza ufanisi wa kuhudumia wananchi.
Hoja ya kutaka jimbo hilo ligawanywe, ilitolewa na Diwani wa Kata ya Mashewa Seif Hillal kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo robo ya pili kilichofanyika Februari 18, 2025 kwenye Makao Makuu mapya ya halmashauri hiyo yaliyopo Kijiji cha Makuyuni, Kata ya Makuyuni, Tarafa ya Mombo.
Wakichangia hoja hiyo baadhi ya madiwani, walisema umefika wakati wa jimbo hilo kugawanywa, sio tu kutokana na wingi wa watu, bali jiografia iliyopo ya jimbo hilo, kwani baadhi ya wananchi wanateseka kupata huduma ikiwemo za kijamii.
“Kutoka kwenye kata yangu ya Kalalani mpaka Makao Makuu ya Wilaya ya Korogwe ni kilomita 130. Halafu kutoka Korogwe hadi Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni kilomita 23, hivyo kuwa kilomita 153.
Watumishi wanaotoka Kalalani kuja Makao Makuu ya Halmashauri wanachukua muda mrefu, na kuwafanya washindwe kurudi kazini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo usafiri, kwani pamoja na kuwepo barabara ambazo wakati mwingine hazipitiki, pia hakuna usafiri wa uhakika.
“Lakini tatizo hilo pia lipo kwenye kupata huduma za afya ngazi ya wilaya, kwani kutoka Kalalani hadi Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni kilomita 153, hivyo kama jimbo likianzishwa hata hospitali yenye hadhi ya wilaya itajengwa ukanda ule, na kuweza kusogeza huduma kwa wananchi” alisema Diwani wa Kata ya Kalalani Amati Ngerera.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe alisema kuomba Jimbo la Korogwe Vijijini kugawanywa ni moja, na kukubaliwa ni jambo jingine. Na alikubaliana na madiwani wenzake kuwa sio kugawanya jimbo tu, hata baadhi ya kata ni kubwa, hivyo pamoja na kupeleka maombi ya kugawanywa Jimbo la Korogwe Vijijini, pia watapeleka maombi ys kugawanywa baadhi ya kata.

“Mimi kama Mwenyekiti wa Halmashauri, kumekuwa na mapendekezo mengi kwa ajili ya kugawa kata ili kuweza kusogeza huduma kwa wananchi. Kuna kata kubwa kwenye halmashauri yetu kama vile Vugiri, Mkalamo, Dindira na Hale. Lakini pia kuna pendekezo la kuugawa Mkoa wa Tanga, ambapo wilaya za Korogwe, Handeni, Lushoto na Kilindi, kuwa na mkoa wao, na Korogwe iwe Makao Makuu.
“Sasa kuomba ni jambo moja, na kukubaliwa ni jambo jingine, lakini sisi kama viongozi, ni lazima tuomba kwa niaba ya wananchi, na kama jambo hilo la kuomba maeneo kugawanywa ikiwemo Jimbo la Korogwe Vijijini na baadhi ya kata litakubaliwa, itakuwa ni jambo jema kwetu na wananchi wetu” alisema Kallaghe.
Akitoa hoja hiyo, Hillal alisema umefika wakati wa kugawa Jimbo la Korogwe Vijijini ili kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi, kwani jiografia ya jimbo hilo baadhi ya wananchi wanashindwa kufikika kwa urahisi na baadhi ya huduma.
“Mwenyekiti, jimbo hili ni kubwa sana, na limeonekana tunapotaka kufikisha huduma kwa wananchi tunakuwa tumempa mzigo mkubwa sana Mbunge wetu Timotheo mnzava. Pendekezo hili linaloletwa najua litahitaji kujadiliwa na kuungwa mkono na baraza hili, lakini najua baada ya baraza hili, Mkurugenzi Mtendaji kuchukua hayo maamuzi na kupeleka kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), kisha kuyapeleka kwa Katibu Tawala wa Mkoa yaani RAS.
“Na yeye RAS atapeleka kwenye kikao cha RCC (Kamati ya Ushauri ya Mkoa), kabla ya kupelekwa kwenye mamlaka nyingine. Vigezo ambavyo vinapendekezwa kugawa jimbo vipo wazi, na kigenzo cha kwanza kikubwa ni mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu. Lakini jambo jingine ni upatikanajj wa mawasiliano, na hali ya kijiografia. Na halmashauri yetu kama mnavyojua wakati ule tulipewa ni kilomita za mraba 3,544, hivyo sijajua kwa sasa kama kuna marekebisho” alisema Hillal.
Hillal alisema kigezo kingine ni masuala ya uchumi, mipaka ya kiutawala, jimbo moja lisiingie kwenye halmashauri mbili, huku akitaja mgawanyo wa Jimbo la Korogwe Vijijini lenye kata 29 kuwa mawili, na kata zake.
“Mwenyekiti, kata ambazo tungependa ziingie kwenye Jimbo la Korogwe Magharibi ni kata ya Mkomazi, Mkalamo, Magamba- Kwalukonge, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni, Magila- Gereza, Lutindi, Lewa na Mlungui.
“Jimbo la Korogwe Mashariki ninapendekeza kata ziwe Dindira, Mpale, Mgwashi, Kwashemshi, Mashewa, Kalalani, Hale, Kwagunda, Mnyuzi, Folofolo, Kizara, Bungu, Magoma, Kerenge na Makumba. Hivyo Mwenyekiti naomba kutoa hoja na madiwani wenzangu waniunge mkono kwa maslahi mapana ya wananchi.” alisema Hillal.

More Stories
Tanzania yajivunia ushirikiano kati yake na Kuwait
Mbunge Mavunde akabidhu mradi wa Shamba kwa wanawake wafanyabiashara wadogo Dodoma
Wasira aihakikishia Marekani uchaguzi nchini kuwa wa huru na haki