December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani wahimizwa kufanikisha uwekezaji eneo la hekta 46,000

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Tanganyika.

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi limetakiwa kuhakikisha uwekezaji kwa ajili ya kilimo,mifugo na viwanda katika eneo la Luhafwe unafanikiwa.

Eneo hilo lilipo kata ya Tongwe linaukubwa wa Hekta 46,000 limetajwa kuwa na fursa ya kukuza uchumi wa watu na halmashauri hiyo kupitia kukusanya mapato.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu katika ukumbi wa halmashauri hiyo wakati akihutubia baraza la madiwani ambapo amesema madiwani wamebeba majukumu kubwa ya mambo  yanayogusa mabadiliko ya kiuchumi na uzalishaji.

Jukumu hilo linatokana na nguvu ambayo baraza la madiwani limepewa na wananchi ya kutunga sera,mipango,usimamizi na uelimishaji umma kwenye masuala ambayo yanahitaji kusukumwa kwa haraka kwa maendeleo ya watu na taifa kama jinsi inavyohitajika kutoa elimu kwa umma kufanikisha uwekezaji katika eneo la Luhafwe bila vikwazo.

Katika eneo la Luhafwe wamepewa wadau  wenye uwezo wa kuwekeza kwenye kilimo,mifungo na viwanda kama vile Suma JKT,ASA,TARI Majinja,Mbozi Highland,Bitendel,Beula,Meru Agro,Seedland,Eco Grain na Mufindi papers mill ambao kwa pamoja watoa fursa kubwa ya kiuwekezaji wilayani Tanganyika.

“Huu mpango tuhakikishe kuwa tunaufanikisha ili uwekezaji tuliotazamia kuuweka pale haupati kikwazo chochote kile kwa sababu ninyi ni wawakilishi wa wananchi tukishikiana kwa pamoja tukaelimishana zoezi hili litakuwa ni jepesi kwetu kwa sababu ndani yake yapo maeneo ambayo mmekaa na kujadiliana kuwa kuna watu ambao wengine watabadilishiwa maeneo yao kwa kupewa mengine,”ameeleza.

Agizo hilo kwa madiwani kutoa elimu kwa wananchi ni baada ya changamoto ya kushindwa kuanza uwekezaji kwa kuwa eneo lilikuwa bado halijapimwa na baadhi ya wananchi takribani kaya 228 kulivamia jambo ambalo halmashauri imechukua hatua ya kutenga eneo jingine linaloendelea kupimwa na hivi sasa zaidi ya hati 48 zimetolewa kwa wananchi hao.

Hamad Mapengo,Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika licha ya kuhakikisha baraza la madiwani litasimamia ufanikishaji wa uwekezaji mkubwa katika eneo la Luhafwe na kwamba faidi nyingi za uchumi zitawanufaisha wananchi kujikwamua kwenye umasikini bali amewataka madiwani hao Kusimamia matumizi ya fedha za serikali kwa ajili ya kuhakikisha fedha za Halmashauri zinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio vinginevyo.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri amesema ili kufuatilia utekelezaji wa mipango yote ya wananchi na ya Halmashauri.Ili kutimiza jukumu hilo ipasavyo, Madiwani wanatakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ndani ya kata  kama inatekelezwa kwa thamani halisi ya fedha zilizotengwa.

Mapengo amesema serikali imeweka fedha nyingi za walipa kodi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo itakuwa jambo la aibu endapo ubadhirifu wa fedha za umma unatokea na wala diwani hafahamu kwani ni wazi diwani huyo atakuwa hafahamu moja ya majukumu yake.

“Twendeni tukakae na wananchi huko vijiji tusikilize kero zao na sio kuzitatua tu bali mkawe sehemu ya ufuatiliaji wa karibu zaidi wa mambo yote yanayotokea huko kwani ni rahisi kubaini ubadhirifu wa fedha za umma kama unatokea kwenye maeneo hayo,”amesema.

Amesema kuwa madiwani wanapaswa kuhamasisha  wananchi kuhusu vita dhidi ya umaskini na katika kulitekeleza hili ni lazima wajue kwa ufasaha hali ya kiuchumi na kijamii inayowakabili wananchi wake na kushirikiana nao ili kupanga mipango endelevu ya kujikwamua.