November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Tabora walaani mwalimu kulawiti mwanafunzi

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Tabora limesikitishwa sana na kitendo cha Mwalimu kumlawiti mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka 7 na kutaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake ili kukomesa tabia hiyo.

Akitoa tamko hilo jana kwenye Kikao cha Madiwani, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Kapela ameeleza kuwa kitendo hicho ni cha kinyama na ukatili wa hali ya juu sana kwa mtoto huyo wa kiume.

Amebainisha kuwa ni aibu kwa mwalimu wa shule kumfanyia ukatili mtoto wa kiume tena mwanafunzi wake, huu ni ukosefu wa maadili wa hali ya juu sana, amemharibia maisha, ni lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

‘Tunalaani sana kitendo hiki, huu ni unyama wa hali ya juu, tabia hii ni lazima ikomeshwe, na akinamama kuweni karibu na watoto wenu, wafuatilieni wanaporudi kutoka shuleni, na wakagueni, wazazi wengi wamejisahau’, amesema.

Kapela amefafanua kuwa mtoto huyo anayesoma katika shule ya St.Dorothy Mjini hapa alibainika kufanyiwa kitendo hicho baada ya miezi kadhaa kupita hali inayoonesha wazazi hawafuatilii watoto wao ikiwemo kuwakagua mara kwa mara.

Amebainisha kuwa wazazi waligundua mtoto wao hakuwa katika hali yake ya kawaida na baada ya kumkagua wakabaini amefanyiwa ukatili huo na alikuwa akitokwa na haja kubwa mfululizo, jambo ambalo liliumiza sana wengi.

Amepongeza kazi nzuri iliyofanya na Vyombo vya Usalama vya Mkoa vikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambaye ni Mkuu wa Mkoa Paul Chacha na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Richard Abwao.

Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Rose Kilimba ameomba jamii kuwafichua wale wote wanaowafanyia vitendo vya ukatili watoto wa kike na kiume ili wakamatwe mara moja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

‘Naomba jamii tusikae kimya, tutoe taarifa ya wale wote wanaowafanyia vitendo vya namna hiyo watoto, tukikaa kimya watoto wataendelea kuharibika, huyu mwalimu ni mfano wa walimu wasio na waadilifu, awajabishwe ipasavyo’, ameeleza.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Malolo, Zinduma Kambangwa alisikitishwa sana na tukio hilo na kuomba serikali kuweka adhabu kali kwa mtu yeyote atakayabainika kubaka mtoto wa kike au kulawiti mtoto wa kiume.