November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Manispaa ya Tabora wamkataa mkandarasi wa barabara

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MADIWANI wa halmashauri ya manispaa Tabora wamemkataa Mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa miradi ya barabara za Mijini na Vijijini katika halmashauri hiyo baada ya kutoridhishwa na ubora wa kazi anazofanya.

Wakichangia hoja ya miradi ya barabara inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) katika wilaya hiyo walisema hawaridhishwi na kazi zinazofanywa na Mkandarasi huyo na hazingatii muda wa kumaliza mradi.

Paul Kananda (diwani wa kata ya Mbugani) alisema TARURA inafanya kazi nzuri lakini huyu Mkandarasi Batalion anawaharibia, barabara zote alizotengeneza katika kata yake hazina kiwango na makalvati aliyojenga yamebomoka.

Alisema thamani ya fedha zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan haiendani na kazi zinazofanyika, barabara zote anazotengeneza katika vijiji mbalimbali hazina ubora na hazidumu, na hana viongozi wakimuuliza hatoi ushirikiano mzuri.

Diwani John Kani (kata ya Kalunde), Chota Charles (Misha) na Salumu Msamazi (Ikomwa) walisema miradi aliyopewa tangu mwaka jana hadi sasa katika kata zao hajaikamilisha na mingine hajaanza hata kidogo kila siku anatoa visingizio tu.

Mhesh. Mwenyekiti hii kampuni ya Batalion haina uwezo, ndiyo maana miradi yote wanayopewa inasuasua, haitekelezwi kwa wakati na hata ikitekelezwa haina ubora, barabara zao nyingi zinaharibika ndani ya muda mfupi’, walisema.

Akitoa azimio la kikao hicho Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela (diwani wa Isevya) alisema hana shaka na utendaji wa Meneja wa TARURA wa Wilaya na Mkoa, wana uwezo mkubwa, ila huyu Mkandarasi anawaharibia.

Alisema licha ya kuaminiwa na kupewa kazi nyingi za miradi ya barabara zinazogharimu mamilioni ya fedha, ameshindwa kuonesha weledi wa kufanya kazi hizo, hivyo hawamtaki, na asipewe kazi nyingine tena katika halmashauri hiyo.

‘Huyu mkandarasi ameipa hasara kubwa serikali, suala la kutekeleza miradi anayopewa chini ya kiwango halikubaliki, tunaomba TAKUKURU wafuatilie mikataba yake yote na miradi aliyopewa na baraza lipewe majibu’, aliagiza.

Akijibu hoja hizo Meneja wa TARURA Wilayaya Tabora Mhandisi Subira Manyama alisema Mkandarasi huyo ni miongoni mwa Wakandarasi 5 waliopewa kazi za ujenzi wa barabara katika manispaa hiyo, na awali alionesha uwezo mzuri.

Alikiri kupokea malalamiko ya madiwani ya kutopewa ushirikiano na Mkandarasi huyo punde wanapofuatilia miradi inayotekelezwa katika kata zao, na kuongeza kuwa Mkandarasi yeyote anapaswa kupokea ushauri na kuufanyia kazi kinyume na hapo atachukuliwa hatua.

Naye Meneja wa TARURA wa Mkoa Mhandisi Edward Lemelo aliwashukuru madiwani kwa kufuatilia kwa karibu miradi ya barabara inayotekelezwa na serikali katika kata zao na kuahidi kuwa atafuatilia suala hilo na kuchukua hatua stahiki.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Tabora Mhandisi Edward Lemelo akizungumzia suala la Mkandarasi (Batalion) anayelalamikiwa na madiwani kwa kutekeleza miradi chini ya kiwango na kutomaliza kazi anazopewa kwa wakati katika kikao cha baraza la madiwani wa manispaa jana. Picha na Allan Vicent.Â