February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Kilindi wapongeza RUWASA utekelezaji miradi ya maji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Kilindi

BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wamepongeza jitihada za Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (RUWASA) kwa kuwapelekea miradi itakayomaliza changamoto ya maji kwa wananchi wao.

Walichokitaka kutoka RUWASA ni kuwa miradi hiyo isisimame ili iendelee kutekelezwa kwa kuhakikisha Wakandarasi ambao kwa sasa wapo kazini, wanaendelea kuwepo hadi miradi itakapokamilika.

Waliyasema hayo Februari 12, 2025 wakati wanachangia taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 iliyotolewa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Diwani wa Kata ya Kisangasa Peter Kunjulu alisema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia RUWASA, kuwa inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji Mgera- Kisangasa, na Mkandarasi yuko kazini anajenga tenki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 na vituo (Vilula) 12, na mradi upo asilimia 80.

Kunjulu alisema, vile vile Mradi wa Maji Kwamaligwa- Gitu unaopeleka maji vijiji saba, kijiji kimoja cha Kwediswati kipo Kata ya Kisangasa. Na kuongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka mashine ya kuchimba visima Wilaya ya Kilindi na sasa  mashine hiyo (Mtambo) ipo Kijiji cha Makingo kwenye Kata ya Kisangasa.

“Miradi ya Maji kwenye Wilaya ya Kilindi inakwenda vizuri. Hata Mradi wa Maji Kwamaligwa ambao utahudumia vijiji saba, na mimi kata yangu ya Kisangasa itapata huduma ya maji kwenye kijiji kimoja cha Kwediswati” alisema Kunjulu.

Naye Diwani wa Kata ya Kilindi Asili, Juma Bewa alisema anaipongeza RUWASA kwa kutekeleza Mradi wa Maji Kilindi Asili, ambapo mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 95 na vituo vya kuchotea maji 34 vimejengwa na tayari vituo 24 vimeanza kutoa maji, na mabomba ya kumalizia mradi yapo eneo la mradi, na mkandarasi anaendelea na kazi.

Bewa ameishauri RUWASA kuendelea kutoa elimu kuhusu Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s) na kuunganishwa uendeshaji wa miradi, mfano mradi wa kata A una mradi wa mtiririko na kata B unaendeshwa na pampu ya umeme, wanajamii wakubaliane ili mradi uwe endelevu.

Mhandisi Odena alisema katika kuboresha  huduma ya maji Vijijini, Wilaya ya Kilindi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imepanga kutumia sh. 4,107,134,678 kwa ajili ya ukamilishaji,uboreshaji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji, ambapo  sh 2,520,191,608 ni fedha za Lipa kwa Matokeo (PforR), sh. 1,566,035,135 za utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maji (NWF), na sh.   20,907,935 fedha kutoka Serikali Kuu (GoT), hivyo kufanya jumla ya fedha za bajeti ya RUWASA Wilaya ya Kilindi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kuwa sh. 4,107,134,678.

“Hadi kufikia robo ya pili 2024/2025 tumepokea kiasi cha sh. 1,348,332,227 toka Serikali Kuu (GoT) na sh. milioni 500 toka Mfuko wa maji (NWF) kwa ajili ya Ujenzi wa miradi ya maji Saunyi (Lombout), Mradi wa Maji Kwamaligwa/Gitu na kufanya jumla ya fedha zilizopokelewa kuwa sh. 1,848,332,227 sawa na asilimia 45 ya bajeti” alisema Mhandisi.

Mhandisi Odena alisema katika uendeshaji wa miradi ya  maji, wilaya  ina jumla ya Bodi nane (8) za Usimamizi wa Miradi   (CBWSO’s) zilizoundwa  kwa kuzingatia  matakwa   ya  sheria  Na. 5  ya Maji  na  Usafi wa Mazingira  ya  mwaka 2019, hivyo miradi yote inayofanya kazi kwa sasa  shughuli za usimamizi, uendeshaji na  matengenezo madogo madogo, zinafanywa na bodi za  usimamizi wa miradi hiyo zilizoundwa.

“RUWASA inaendelea  kutoa  mafunzo  kwa bodi  hizi  ili  zifanye  kazi  yake  kwa ufanisi  na weledi   na  kuhakikisha  kuwa  miradi ya maji   inakuwa  endelevu  na kutoa  huduma  bora  kwa  wananchi.
Waziri wa Maji (Jumaa Aweso) anasimamia miradi yote nchi nzima, na  ndoto ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuunganisha CBWSO za Maji nchi nzima kama mtandao wa TANESCO” alisema Mhandisi Odena.