November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madini ana kwa ana na Wadau

Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko amesema kupitia Jukwaa la Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma,wizara yake itakaa na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Madini ikiwemo ucheleweshwaji wa majibu ya sampuli za madini katika maabara yao na kuona namna ya kuzitatua.

Waziri Biteko Kauli hiyo jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Wiki ya Utumishi wa Umma ambapo wizara hiyo imeaanda jukwaa la maonyesho ili wananchi na wadau mbalimbali waweze kutembelea na kujifunza.

Aidha, amesema mfumo wa utoaji huduma katika wizara hiyo, umebadilika zaidi na hivyo kuwataka wateja ambao ni wananchi na wadau kufika katika maonyesho hayo kujifunza ikiwa ni pamoja na kutoa kero zao ili waweze kuzifanyia kazi.

Amesema lengo la wiki ya maadhimisho ya utumishi wa umma ni kuwezesha kuboresha mchakato wa utoaji huduma kwa mteja na wao kama wizara hiyo ni fursa kwao huku akisema wanatarajia kukutana na wachimbaji wadogo na wakubwa kwakufanya nao kikao kukaa na kuzungumza nao kujua changamoto zao.

Kwa upande wake,Jackline Aloyce ambaye ni Afisa Utumishi Mwandimizi wa Wizara ya Madini ameeleza lengo la maadhimisho hayo kuwa ni kutoa huduma bora kwa wateja ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na malalamiko ya wateja.

“Kupitia maonyesho haya tumeandaa majukwaa katika Taasisi mbalimbali ikiwemo ofisi za Mtumba ili kutoa elimu kwa wadau mbalimbali lengo na wao kutoa maoni kero na ushauri ili tuweze kuzifanyia kazi,”amesema.

Akizungumza katika maonyesho hayo mmoja wa wateja, Kulwa Kitine amesema kumekuwa na ucheleweshaji wa majibu katika upimaji sampuli za madini na hivyo kuiomba wizara kutatua changamoto hiyo ili kujenga imani kwa wateja wao.

“Sampuli zimekuwa zikichukua muda mrefu jambo ambalo limepelekea wateja kutokuwa na imani na sisi na hivyo wakati mwingine kuama kupeleka sampli zetu mikoa mingine ikiwemo Geita,”amesema.

Maadhimisho hayo ya Wiki ya Utumishi wa Umma Nchini yanaratibiwa na Ofisi ya Rais Utumishi ambapo katika wizara hiyo yameandaliwa na Taasisi ya Uhamasishaji,Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini,Mafuta na Gesi asilia ambayo yameanza Juni 16 na kilele chake ni Juni 23, mwaka huu.