December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkazi wa Tabora akipatiwa huduma ya Kinywa na Meno na Madaktari Bingwa katika hospitali ya rufaa ya Kitete Mkoani Tabora

Madaktari bingwa 45 wa Rais Samia kutoa huduma Pwani

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Pwani

MADAKTARI Bingwa wa Mama Samia 45 wamepiga kambi Mkoani Pwani kwa siku tano ili kutoa huduma za afya za kibobezi kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo ya uzazi na matibabu kwa watoto.

Aidha, watatoa huduma kwa wagonjwa ya wanawake ,dawa za usingizi ,upasuaji wa kibobezi, magonjwa ya kawaida na kutoa rufaa kwa wale watakaohitajika.

Akizungumza na madaktari bingwa hao katika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge alieleza kuwa udaktari ni kazi ya wito na kujitolea kuokoa maisha ya watu .

Aliwataka madaktari hao kutoa huduma bora kwani wameaminiwa na ni kazi iliyobeba maisha ya watu.

Kunenge ametoa rai kwa wataalam wa afya na madaktari kwenda na mabadiliko ya kidunia kwa kuwa wabunifu na watafiti ili kupanua uelewa na kutoa huduma bora na Kwa utaalamu zaidi.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya ,kuongeza vifaa tiba ,madawa na miundombinu ili kutoa huduma bora kwa watanzania .

“Serikali imekuwa ikihakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema, hivyo amekuwa akielekeza raslimali fedha ili kujenga majengo, hospital kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alieleza Kunenge.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani (RMO) Dkt.Benedicto Ngaiza, alisema ,wamejipanga na walianza maandalizi ya ujio huo tangu wiki iliyopita.

“Hamasa ni kubwa, tunatarajia wananchi wengi watajitokeza kupatiwa huduma na kupata tiba stahiki”

Ngaiza alifafanua,Kuna maeneo yenye changamoto ya masuala ya ukatili, jamii ikimbilie fursa hiyo kufichua waathirika wa changamoto walizozipata ili wapewe huduma.

Vilevile, mganga mkuu huyo alieleza kati ya magonjwa wanayoongoza kwa sasa mkoani Pwani ni ugonjwa wa malaria na magonjwa ya njia ya hewa ambayo yametokana na hali ya hewa iliyopo.

Hata hivyo Ngaiza alieleza, magonjwa yasiyoambukiza yanayoongezeka ni shinikizo la juu la damu, kisukari na figo.

Ofisa mradi kutoka wizara ya afya, John Meena anasema madaktari hao watakuwa Pwani kuanzia Juni 3 hadi Juni Juni 7 mwaka huu.

Alifafanua, kampeni hiyo ya madaktari wa Samia kutoa huduma kwa wananchi ni zoezi Endelevu.

Mkoa wa Pwani una wilaya saba, Halmashauri Tisa, ina jumla ya Hospital 13 kati ya hizo Rufaa ya Mkoa Tumbi, vituo vya afya 50, kliniki za kutoa Huduma za kujifungulia 22 na zahanati 388.