Na Catherine Sungura,TimesMajira online
UPANUZI wa huduma za kibingwa na kibobezi kupitia wataalam mbalimbali wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) ni miongoni mwa mambo yaliyotiliwa mkazo na uongozi wa hospitali hii.
Ndani ya kipindi cha miaka mitano,MZRH imeimarisha na kuboresha huduma muhimu nane za kibingwa zinazotolewa kwa wananchi wa mikoa saba (7) ya Nyanda za juu Kusini (Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa na Katavi).
Mkurugenzi Mtendaji wa MZRH Dkt.Godlove Mbwanji,anataja huduma hizo ni pamoja na huduma za magonjwa ya ndani, magonjwa ya moyo na mishipa ya fahamu, mfumo wa hewa, figo, ngozi, damu na saratani.
Anataja huduma nyingine ni Methadone kwa waathirika wa madawa ya kulevya ambapo Huduma zilianza kutolewa July 2017 kwa waathirika wa madawa ya kulevya 6 na sasa tuna hudumia wagonjwa zaidi ya 245 kwa ukanda huu. Hawa wote wamerudi kwenye majukumu yao ya kawaida ya uzalishaji/kufanya kazi na kuhudumia familia zao.
Maboresho mengine ni katika Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, kuanzishwa kwa kiwanda cha maji-tiba (Infusion Unit) ambayo huzalishwa kwa asiliamia 78 ya uhitaji wa matumizi ya hospitali na upatikanaji wa huduma ya viungo mbadala na vifaa tiba saidizi(Prosthetics and Orthotics).
MAABARA
Anasema Maabara ya hospitali hiyo yenye ithibati (accreditation) ya kimataifa imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za maabara kwa kuongeza vitengo kutoka vitatu vya Immunohistochemistry, Serology na Haematology hadi kufikia tisa.
“Tuna maabara ya kisasa iliyopewa Ithibati “Accredation” yenye uwezo wa kufanya vipimo katika ngazi ya kimataifa pia ina uwezo wa kupima magonjwa ya Ebola na mengine yanayofanana na hayo –Dkt Mbwanji
Anataja vitengo hivyo ni Hematology, Molecular biology, Parasitology, Bacteriology, TB, Blood Transfusion, Serology,Immunophenotyping (CD4 lab) na Clinical chemistry.
RADIOLOGIA
Dkt. Mbwanji,anaeleza kuwa idara ya imeboreshwa zaidi kwa Upatikanaji wa huduma za mionzi kama CT Scan, mashine za kidigitali za X ray, Fluoroscopy, Mammography na Ultrasound. Hii imemwezesha mwananchi wa kipato cha chini kueza kumudu vipimo hivi kutoka na gharama za vipimo tajwa kuwa nafuu, awali mwananchi alikua asafiri umbali mrefu kufwata huduma hizi ambapo zilikua zikipatikana jijini Dar es Salaam.
DAWA
“Upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 96 hadi 98, hii ni kutokana na kuanzishwa kwa vitengo vipya vya magonjwa ya saratani na damu.
“Sasa dawa zote muhimu zinazohitajika zinapatikana kwa kufuata mwongozo tiba wa Taifa na uzoefu wa wataalamu, madaktari,” anasisitiza.
MIKOA INAYOHUDUMIWA
Dkt. Mbwanji anasema wanahudumia Kanda ya Nyanda za juu Kusini yenye mikoa saba (7) ikiwamo; Mbeya, Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Njombe na Songwe yenye jumla ya watu wapatao milioni nane (8,000,000).
“Hospitali imegawanyika katika maeneo makuu matatu, Hospitali Kuu, Hospitali ya Wazazi Meta na Kitengo cha Watoto,” anabainisha Dkt. Mbwanji.
Anasema hospitali hiyo majukumu yake makuu ni kutoa huduma za Tiba, Mafunzo kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu pamoja na kufanya Utafiti.
“Tumeweza kutoa mafunzo ya Udaktari katika ngazi ya shahada kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa sehemu ya Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa chuo kina takriban wanachuo 1, 000,” anasema.
Anasema hospitali ina jumla ya vitanda 603, inahudumia wagonjwa wa nje na wagonjwa wa ndani.
Anasema katika kipindi cha Julai 2020 hadi Februari 2021, walihudumia jumla ya wagonjwa 225,548, kati yao wagonjwa wa nje walikuwa 194,345 na wa ndani 31,203.
Anaongeza “Wapo watumishi 893 wa kada mbalimbali, 670 kati yao wameajiriwa na Wizara na 223 wameajiriwa na hospitali kwa mkataba kwa malipo ya fedha zinazokusanywa ndani.
“Kuna madaktari 108 katika fani mbalimbali kati yao 56 ni madaktari bingwa, Wafamasia wanane, Wateknolojia Dawa 10, Wateknolojia maabara 25, Wauguzi 198 na Wasaidizi Afya 238.
Anasema watumishi hao wanatoa huduma katika Idara mbalimbali za hospitali ikiwamo ya upasuaji, tiba, wagonjwa wa nje na dharura.
“Wagonjwa wa afya ya akili, mionzi, wazazi, famasi, macho, maabara, kinywa na meno, fiziotherapia, watoto, utawala, uhandisi, uhasibu na ugavi,” anabainisha.
WAMEOKOA MAISHA
Dkt. Mbwanji anasema kuboreshwa kwa huduma za MZRH zikiwemo za matibabu ya saratani na figo zimesaidia kuokoa maisha ya Watanzania, kwani awali wengi walizikosa katika ukanda wa nyanda za juu kusini na kupelekea kufariki dunia.
Anataja faida nyingine za uwazishwaji wa huduma hizo MZRH ni pamoja kuwapunguzia gharama na umbali wa kufuata huduma wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya jirani katika ngazi ya Taifa kama vile Muhimbili, MOI na Ocean Road.
“Kwa sasa wagonjwa wanao uwezo wa kusafiri kutoka mikoa iliyopo katika kanda na kurudi bila mashaka kutokana na kuwepo huduma nyingi za kibingwa na vipimo katika hospitali yetu,” anabainisha.
HUDUMA ZA KIBINGWA
Anasema wamefanikiwa kutoa huduma za kibingwa, kama upasuaji wa kawaida na upasuaji kwa njia ya vitundu “Laparascopic Surgery” pamoja na upasuaji wa tezi dume kwa njia ya vitundu (TURP, TURBT) usafishaji wa figo (haemodialysis) na huduma za kibingwa za masikio, koo, pua (E.N.T) ambapo kwa wiki operesheni za pua 15-25 zinafanyika.
Anaongeza “Tumeboresha huduma kwa kutumia mfumo wa kieletroniki (eMedical) na kuweza kusaidia katika kudhibiti upotevu wa mapato jambo linalopelekea hospitali iweze kujiendesha kwa mapato ya ndani.
“Tumeanzisha huduma ya Mkalimani wa lugha za alama jambo ambalo limepelekea mafanikio kwa Taasisi na Jamii kwa ujumla ambapo zaidi ya viziwi 300 kutoka ukanda huu wanapata huduma ni hospitali pekee nchini Tanzania kuanzisha huduma hii baada ya kuona WATU viziwi washindwa kupata uhuduma stahiki za matibabu kutokana kukosekana kwa mawasiliano mazuri kati ya mgonjwa, daktari na watoa huduma wengine.,” anasema.
Anasema kupitia Mkalimani wameweza kutoa huduma ya Tohara kwa wanaume viziwi wapatao 25 na kuweza kupata elimu ya kupambana na maambukizi ya UKIMWI.
“Tumeweza kutoa huduma ya upasuaji mkubwa kwa viziwi 6 na kutoa huduma ya elimu ya uzazi wa mpango na kuepusha mimba zisizotarajiwa kwa watu wenye matatizo ya kusikia,” anasema.
TANZANIA YA VIWANDA
Anasema katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuelekea Tanzania ya Viwanda, Hospitali imeboresha miundombinu kwa kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa MAJI TIBA‘Dripu’ za IV(Intravenous Fluids) tiba zenye ujazo wa mil’s 250 na Mil’s 500 hali inayo sababisha kuondokana na adha ya kununua\kuagiza dripu nje ya nchi.
“Kiwanda kimekamilika na uzalishaji maji tiba umeshaanza, kwa siku kiwanda kinazalisha lita 120 za maji hatua inayofuata tumeanza maandalizi ya mpango wa kutengeneza dawa za macho.’ anabainisha.
Anasema wametengeneza mfumo wa TEHAMA (eMedica) kwa kutumia wataalam wa ndani na “Saver” ya mfumo huu ipo ndani ya hospitali, umesaidia kupunguza gharama za uendeshaji.
Anaongeza “Awali tulitumia mfumo wa Care2X uliogharimu fedha nyingi kwa matengenezo na maboresho ya mfumo, tulilazimika kugharamia wataalam kutoka Arusha na Morogoro.
“Pamoja na mfumo huu, wataalam wa TEHAMA walioajiriwa na hospitali, wamefanikiwa kutengeneza mfumo wa “Nursing call”, mgonjwa akihitaji usaidizi wa muuguzi anabonyeza kitufe na muuguzi anajua anahitajika kutoa msaada kwa mgonjwa yupi.
“Mafanikio mengine ni uwepo wa wahandisi wa vifaa tiba, ambao wameweza kufanya marekebisho ya vifaa tiba mbalimbali ndani ya hospitali, kwa wakati bila kuhitaji msaada kutoka nje ya taasisi. Hii imesaidia kupunguza gharama za uendeshaji,” anabainisha.
MIPANGO YA BAADAE
Dkt. Mbwanji anasema wataboresha huduma katika Divisheni ya Tiba na Uchunguzi, pamoja na kupanua huduma za kibingwa na kibobezi kwenye maeneo mbalimbali hasa yale ambayo kwa sasa hazipo.
“Kama vile magonjwa ya mfumo wa chakula (Gastroenterology), mfumo wa fahamu (Neurology) na huduma za kibobezi kwa watoto kama vile huduma za magonjwa ya moyo kwa watoto (Padiatric cardiology).
“Tutaboresha huduma za Radiolojia kwa kusimika machine ya MRI, ambayo tunatarajia kupatiwa na Wizara kupitia mradi wa ORIO.
“Tutapanua huduma za magonjwa ya Saratani kwa kuanzisha huduma za mionzi na kuboresha zile za utoaji wa dawa za saratani na huduma za maabara.
“Tutaimarisha utoaji huduma za Histopatholojia zenye ithibati (accreditation) ambapo itafanya upatikaji wa dawa kutoka asilimia 98 mpaka kufikia asilimia 100.
MIRADI INAYOENDELEA
Anasema Serikali imetenga bajeti ya sh.Bilioni 9.151 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya kisasa ya Wazazi Meta ambayo ni sehemu ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ambalo linatarajiwa kukamilika ifikapo April 30, 2021.
“Kasi ya ujenzi ni nzuri na tayari umekamilika kwa asilimia 80, jengo litakuwa na uwezo wa vitanda 223” anasisitiza.
“Tutaanzisha pia huduma za upasuaji wa mgongo na mishipa ya fahamu kwa kusomesha wataalaam, ukarabati wa vyumba vya upasuaji, pamoja na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba,” anasema.
CHANGAMOTO
Anataja baadhi ya changamoto zinazowakabili ni upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali kwa asilimia 32.
“Upungufu mkubwa upo kwa kada za madaktari Bingwa, madaktari na wauguzi, ili kukabiliana nayo, hospitali imeajiri watumishi 223 wanaolipwa mishahara kwa mapato ya ndani,” anasema.
Anaongeza “Pia, hospitali kwa kupitia Wizara inapeleka wataalam kwenye mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili kukabiliana na upungufu huu.
“Aidha, hospitali imeweza kukopa fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya kujenga mtambo wa kuzalishia gesi ya oksijeni “oxygen plant” katika mwaka wa fedha 2020/2021.
VIWANGO KIMATAIFA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima anasema hatua ya maabara ya MZRH kuwa na uwezo wa kuchunguza sampuli kwa viwango vya kimataifa ni ya kupongezwa, licha ya changamoto kadhaa ambazo bado zinawakabili.
“Hili ni jambo jema kwa sababu huduma za afya bila kuwa na viwango inakuwa kidogo haziaminiki. Hospitali hii mmeweza kufanya jambo kubwa mno,
“Huu mfumo wa TEHAMA ambao mmeutengeneza ninyi wenyewe, kupitia wataalamu wazawa hili nalo ni ‘innovation’ kubwa ya watu walioamua kufanya mabadiliko,” anasema.
Anaongeza “Hivi sasa tunayo mifumo mingi ya TEHAMA inafanyiwa sensa, yote tunataka tuje na mifumo michache ambayo imetengenezwa na wazawa ili iweze kukuzwa, lakini kubwa iweze kuongea.
“Mfumo wa Mbeya uweze kuongea na wa Muhimbili hilo ndilo tunaloliangalia ili ‘tusiwa-discourage’ (tusiwavunje moyo) wazalendo ambao wameamua kuipambania sekta ya afya kuhakikisha tunachohudumia hapa si lazima mtaalamu atoke nje ya nchi.
“Itoshe kusema kwamba Mbeya hata sasa nimekuwa sina shaka na asili ya kiongozi mliyenaye na timu mliyonayo ni watu ambao wakiagizwa kitu wanakifanya, hongereni na muendelee hivyo,” anatoa pongezi, rai.
Sambamba na hayo, Dkt. Gwajima anawataka watumishi wa hospitali hiyo kuendeleza uzalendo na kuhakikisha wanazilinda vema rasilimali za Umma.
Waziri huyo anahimiza pia kuimarishwa kwa mfumo wa dawa kuhakikisha kunakuwa na mfumo madhubuti wa kutambua dawa inapoingia hadi inapomfikia mgonjwa.
“Haiwezekani tuwe na maswali yasiyo na majibu, mwingine mali imeingia taarifa haionekani, mwingine alipokea bidhaa ikaingia kwenye kumbukumbu, lakini hazijawahi kutoka stoo kwenda kwenye amaeneo ya huduma, hazipo na maelezo hana.
“Eti alipewa mwanafunzi, alipomaliza ‘intern’ hakuna, hizo hadhithi hazipo, wakati wa kujulikana mali ya serikali nani ameitumia ni huu.
“Mwingine anatoka nje ya mfumo wa MSD,lakini hana hati yoyote ya kusema kwamba mimi MSD sina, ameenda kununua bidhaa mwezi wa saba mwaka ule ametumia hati ya Januari,mwaka ule ambayo ‘imeshaexpire’
“Hawa pia wapo, hatuna uvumilivu nayo,kila aliyelitengeneza, akalikoroga ajiandae tu kulinywa, ni suala la muda, kwa hiyo sitaki taarifa yenu nzuri niondoke hapa nisieleze hizi habari mkaja mkatumbukia humo,” anahimiza.
Anaongeza “Kama mlifanya kabla ya kukaguliwa mtapongezwa,kama mlikuwa mnafanya mjitoe kabisa kwenye hizi taratibu zinazoturudisha nyuma katika matumizi ya rasilimali za umma.
More Stories
Hivi ndivyo TASAF ilivyoshiriki kumaliza kilio cha wananchi Kata Bwawani, Arusha
Mfumo unavyokwamisha wanawake kuwa viongozi
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni