November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maboresho bandari ya Tanga yaleta matokeo chanya sekta ya usafirishaji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kufuatia kukamilika kwa maboresho makubwa ya miundombinu katika Bandari ya Tanga, wadau katika sekta ya usafirishaji nchini wameanza kuitumia kusafirisha bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Wadau hao wamebainisha kwamba maboresho hayo makubwa yaliyofanyika katika Bandari hiyo yameshawishi Meli kubwa na kisasa zilizokuwa zinatumia Bandari shindani za nchi Jirani kuanza kuleta Meli zao katika Bandari ya Tanga

Kwa sasa meli zote kubwa ambazo zinahudumiwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki, hivi sasa zinaweza kuhudumiwa katika Bandari ya Tanga, amesema Masoud Mrisha, Meneja wa Bandari ya Tanga.

Mafanikio hayo yanajiri ikiwa ni baada ya kampuni ya usafirishaji ya Simba Terminals kushawishi moja ya ya Meli kubwa na ya kisasa kutumia Bandari ya Tanga kusafirisha Shehena ya mzigo wake kutokea nchini Urusi ikielekea nchini Congo DRC.

Meneja wa Kampuni hiyo ya Simba Terminals, Bw. Awadhi Massawe amesema kuwa jumla ya tani 4900 za kichele zimeshushwa bandarini hapo na Meli hiyo ya mizigo.

Naye Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Masoud Mrisha amesema kuwa meli zimeanza kuja kwa wingi katika Bandari ya Tanga mara baada ya maboresho makubwa kufanyika ambapo sasa meli inashushia mzigo kwenye gati tofauti na mwanzo ambapo zilikuwa zikishushia nangani.

“Hadi sasa Bandari ya Tanga imeshahudumia takribani meli kubwa 19 kutoka nchi mbalimbali Duniani zikija na Shehena ya mzigo wa zaidi ya tani laki moja”, amesema Mrisha.

Kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 bandari ya tanga inalenga kuhudumia mizigo tani milioni 1.2.

Maboresho ya kimkakati yaliyofanyika kwenye bandari hiyo, kwa ujumla yamegharimu kiasi cha shilingi bilioni 429.1 za Kitanzania.

Maboresho yaliyofanyika ni pamoja na kuongeza upana wa mlango bahari, sehemu ya kuingia na kutoka meli (entrance Channel), kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi mita 13, kuongeza sehemu ya kugeuzia meli (turning base), na upanuzi wa magati mawili kufikia upana wa mita 450.

Bw. Mrisha amebainisha kuwa, bandari hiyo kwa sasa ufanisi wake umeongezeka ikiwemo kutumia muda mchache kuhudumia meli, gharama za uendeshaji kupungua, hali iliyopelekea idadi ya meli zinazohudumiwa katika bandari hiyo kuongezeka.

“Sasa hivi Kuna meli kubwa, BSL NODIC yenye uwezo wa kubebea tani 4,967 na urefu wa mita 169.26 ambayo inahudumiwa, ambapo tumepanga kuihudumia kwa shift 5, hapo awali meli hii ingehudumiwa kwa shift 10” alisema Mrisha

Kuhusu mpango wa kuanza kupokea meli ya magari katika bandari ya Tanga, Meneja Mrisha amesema,
“Wiki iliyopita tumekutana na shipping line (wadau wa usafirishaji kupitia meli) wenye ubia na kampuni ya Mitsui, tumefanya mazungumzo nao, na wamesema wako katika mpango wa kuleta meli ya magari hivi karibuni katika bandari ya Tanga, na hapo awali jambo hilo lingekuwa ni kitendawili. Tutapokea meli za magari kuanzia sasa” alihitimisha Mrisha.

Bandari ya Tanga ni kati ya Bandari tatu kubwa zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. Ndio Bandari ya pili kwa ukubwa.

Bandari nyingine katika Ukanda huo ni pamoja na Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio Bandari mama na Bandari ya Mtwara ambayo ni tatu kwa ukubwa.